Wananchi wamehimizwa kutembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane 2026 ili kujifunza teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dkt. Ismael Kimirei, wakati akizungumza na waandishi wa habari Agosti 1, 2026 katika viwanja vya maonesho hayo jijini Dodoma.

Dkt. Kimirei amesema mwaka huu TAFIRI imekuja na teknolojia mpya ikiwemo kitotoleshi cha samaki kinachohamishika kutoka eneo moja kwenda jingine, kilichobuniwa na watafiti wa Kituo cha TAFIRI Jijini Mwanza, amesema kitotoleshi hicho kinaweza kuunganishwa na kifaa cha kupima ubora wa maji, ikiwemo kiwango cha joto na oksijeni, ambavyo ni muhimu katika ufugaji wa samaki kwenye vizimba au mabwawa.

Aidha, amesema taasisi hiyo inaonesha teknolojia ya uzalishaji wa Spirulina yaani vimea maji vinavyopatikana katika maji yenye kiwango kikubwa cha chumvi kama Ziwa Natron, na Kwa mujibu wa tafiti, Spirulina ina zaidi ya asilimia 62 ya protini pamoja na virutubisho vingine muhimu kwa afya ya binadamu.

Ameeleza kuwa Spirulina hutengenezwa katika mfumo wa unga na vidonge na inaweza kutumika kwenye uji, supu na vyakula vingine, ikiwa ni njia ya kuongeza upatikanaji wa virutubisho muhimu hususan kwa wanawake na watoto.

Pia amesema TAFIRI imebuni mitambo ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, ikiwemo kaushio la dagaa linalotumia mwanga wa jua, ambalo husaidia kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi na kuongeza kipato kwa wavuvi na waongezaji thamani wa mazao hayo ya uvuvi.

Mbali na hayo, amesema banda la TAFIRI linaonesha samaki wa mapambo wenye thamani kubwa katika soko la kimataifa, ambao pia husaidia kupendezesha mazingira ya nyumbani na kuwajengea watoto utamaduni wa kutunza mazingira.

Dkt. Kimirei amesisitiza wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Nanenane kutembelea banda la TAFIRI ili kupata elimu na maarifa kuhusu tafiti, ubunifu na teknolojia zinazochochea maendeleo ya sekta ya uvuvi nchini.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...