Na Janeth Raphael - Michuzi TV

Serikali imeanzisha vituo maalumu vya huduma za dharura na kituo cha mawasiliano kwa wakulima (Call Centre) katika Maonesho ya Nanenane 2026, hatua inayolenga kuimarisha huduma za kilimo, kukabiliana na majanga yanayotokea mashambani pamoja na kuwasaidia wakulima kutambua mbegu halali na kuondokana na matumizi ya mbegu bandia.

Hatua hiyo ni sehemu ya maboresho makubwa yaliyofanywa katika maonesho ya mwaka huu yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, chini ya kaulimbiu "Jenga Kesho Iliyo Bora."

Akizungumza katika maonesho hayo, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Nanenane 2026 yanakuwa zaidi ya maonesho ya bidhaa, bali ni jukwaa la kutoa elimu, kutatua changamoto za wakulima na kuwaunganisha na huduma muhimu zitakazoongeza tija katika sekta ya kilimo.

Amesema kituo cha huduma kwa wakulima kitawawezesha wakulima kupata taarifa sahihi kuhusu ubora wa mbegu walizonunua, kubaini kama ni halali au bandia, pamoja na kupata elimu kuhusu teknolojia za kisasa na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa njia ya kidijitali.

"Wakulima watapata nafasi ya kuuliza na kupata taarifa sahihi kuhusu mbegu walizonunua kama zina ubora unaotakiwa au la. Pia watapata ufafanuzi kuhusu huduma mbalimbali za kilimo zinazotolewa kwa njia ya mtandao," alisema Chongolo.

Aidha, amesema Serikali imeanzisha kituo maalumu cha kushughulikia majanga ya kilimo kitakachopokea taarifa za dharura kutoka kwa wakulima na kuratibu hatua za haraka pindi changamoto zinapojitokeza.

Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na uvamizi wa nzige na wadudu wengine waharibifu ambao wamekuwa wakisababisha hasara kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

"Tumekuwa tukishuhudia changamoto mbalimbali kama uvamizi wa nzige ambao wakati mwingine husababisha hasara kubwa kwa wakulima. Kituo hiki kitasaidia kutoa majibu ya haraka pale majanga yanapotokea," alisisitiza.

Mbali na vituo hivyo, Serikali pia imeweka kituo cha huduma za ugani kitakachowaunganisha wakulima na wataalamu wa kilimo ili wapate ushauri wa kitaalamu kuhusu uzalishaji wa mazao, matumizi sahihi ya mbegu bora, viuatilifu pamoja na mbinu za kisasa za kuongeza tija.

Chongolo alisema taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), pamoja na wadau wa sekta hiyo, zimejipanga kutoa elimu na teknolojia zitakazowawezesha wakulima kuzalisha kwa ufanisi zaidi.

Alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kilimo ili kuwaunganisha wakulima, hususan vijana, na masoko, wataalamu pamoja na taarifa muhimu zinazowasaidia kufanya kilimo chenye tija na faida.

"Tunataka vijana waone kilimo kama fursa ya kiuchumi. Kupitia teknolojia wataweza kupata taarifa, masoko na huduma zitakazowawezesha kuzalisha kwa tija," alisema.

Aidha, alisema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwaunganisha wakulima na masoko ya uhakika pamoja na kutoa elimu ya matumizi salama ya viuatilifu ili kuongeza ubora wa mazao na ushindani wa bidhaa za kilimo.

Maonesho ya Nanenane 2026 yanafanyika katika kanda nane nchini na yanalenga kuonesha fursa zilizopo katika sekta ya kilimo, hususan kwa vijana wanaozidi kujitokeza katika shughuli za uzalishaji na biashara ya mazao.

Kwa mujibu wa Waziri Chongolo, maandalizi ya maonesho ya mwaka huu yalifanyika kwa takribani miezi 12, yakilenga kufanya Nanenane kuwa jukwaa la kudumu la ubunifu, teknolojia na maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...