Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka, amewataka wakazi wa Dodoma, mikoa jirani na Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho ya kilimo Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nanenane jijini Dodoma na kutembelea Banda la Kijiji cha Ushirika.

Chitinka amesema Banda hilo limeandaliwa kwa mara ya tatu mfululizo na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Ushirika TFC kwa lengo la kuonesha bidhaa, shughuli mbalimbali pamoja na huduma zinazotolewa na vyama vya ushirika nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 1, 2026 katika viwanja vya Nanenane jijini Dodoma, amesema Banda la Kijiji cha Ushirika ni jukwaa maalum linalowakutanisha wadau wa sekta hiyo na kutoa fursa kwa wananchi kufahamu mchango wa vyama vya ushirika katika maendeleo ya kiuchumi.

Amesema kupitia Banda la Mkoa wa Dodoma linaloratibiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Dodoma (DORECU), wananchi wataweza kuona mazao 12 yanayooneshwa, yakiwemo ufuta, choroko na mbaazi.

Aidha, amesema wananchi watapata elimu kuhusu taratibu na sifa za kujiunga na vyama vya ushirika, hususan vya mazao, pamoja na fursa za mikopo zinazopatikana kupitia ushirika.

“Maonesho haya yatasaidia wananchi kufahamu namna vyama vya ushirika vinavyomuinua mkulima, kuongeza kipato na kumsaidia mwananchi kujikwamua kiuchumi,” amesema Chitinka.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Dodoma unajivunia mchango wa sekta ya ushirika katika kuchochea maendeleo ya wananchi, huku ukiendelea kusimamia kauli mbiu ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu.”




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...