Serikali imejipanga kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo ya Polio ili kuendelea kuilinda Tanzania dhidi ya ugonjwa huo, licha ya nchi kutokuwa na mgonjwa wa Polio kwa sasa.

Hayo aliyasema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri katika hafla fupi ya ufunguzi wa kampeni ya utoaji chanjo ya Polio iliyofanyika katika Shule ya Msingi Nkuhungu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Alhaj Shekimweri alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha afya za watoto nchini, akieleza kuwa watoto wamekuwa sehemu muhimu ya programu mbalimbali za afya zinazotekelezwa na serikali.

Aliongeza kuwa kama Wilaya ya Dodoma imepewea lengo la kuwafikia watoto 207,096 katika zoezi hilo, ikiwa ni sehemu ya jumla ya watoto 1,003,061 katika Mkoa wa Dodoma wanaolengwa katika maeneo husika.

“Viongozi, watendaji wa serikali, shule, kamati na bodi za shule wamehamasishwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo, ikiwamo kuwafikishia wazazi ujumbe kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto kupata chanjo ingawa hatuna changamoto ya mgonjwa wa Polio nchini, ni muhimu kujihami kwa kuwakinga watoto wetu,” alisema Alhaj Shekimweri.

Kwa upande wake, mkazi wa Dodoma, Rosmith Mkoko aliishukuru serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo hiyo, akiwataka wazazi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo.

“Chanjo ni muhimu katika kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa na kwamba wazazi wanapaswa kutumia fursa hii kuhakikisha watoto wao wanapata kinga. Nawashauri wazazi wawalete watoto wapate chanjo hizi ili ziweze kuwalinda,” alisema Mkoko.

Zoezi hilo linatarajiwa kuendelea hadi tarehe 30 Agosti, 2026 kwa kushirikisha jamii, hususani wazazi na walezi, ili kuhakikisha watoto wote waliolengwa wanapata chanjo kwa wakati.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...