HALMASHAURI ya wilaya ya Siha inatarajia kutoa chanjo ya ugonjwa wa Polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10 wapatao 42049 ambapo wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha zoezi hilo linawafikia watoto wote walengwa ili kukabiliana na ugonjwa wa Polio.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Christophe Timbuka wakati wa uzinduzi uliofanyika katika shule ya msingi Wiri ambapo kampeni hiyo itafanyika kwa siku nne na kudai kuwa, serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuimarisha na kulinda afya za wananchi hususan afyavna usalama wa watoto.
Dkt. Timbuka alisema kuwa, ugonjwa wa Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya Polio ambapo huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha kupooza kwa viungo na hivyo kupelekea ulemavu wa kudumu.
"Jambo la msingi mnalopaswa kuelewa ni kwamba Polio inazuilika kwa chanjo na ndio maana Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha watoto wote walio katika kundi lengwa la umri chini ya miaka kumi wanapatiwa chanjo kwa wakati" alisema Dkt. Timbuka.
Alisema kuwa, Tanzania imeendelea kulinda mafanikio yake katika mapambano dhidi ya Polio, lakini bado tunapaswa kuwa waangalifu kutokana na uwepo na mzunguko wa virusi vya Polio katika baadhi ya maeneo ya Afrika na duniani.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe inasisitiza kuwa, kampeni ya chanjo kwa watoto chini ya miaka 10 ni sehemu ya juhudi za kuongeza kinga ya jamii na kuzuia uwezekano wa maambukizi kwa hiyo, kampeni hiyo siyo jambo la kawaida la utoaji wa huduma za afya, bali ni juhudi ya kitaifa ya kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya ugonjwa unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu na kupoteza nguvu kazi ya taifa letu.
Alibainisha kuwa, chanjo hiyo itatolewa katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa na timu ya wataalamu wa afya pamoja na wahamasishaji waliopata mafunzo watatoa chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya, Shule za Awali na Msingi, vituo vya malezi ya Watoto (Daycare), Makao ya Watoto, Maeneo ya mikusanyiko ya jamii, huduma za nyumba kwa nyumba na Maeneo mengine yatakayobainishwa katika mpango kazi wa Halmashauri za vijiji.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Siha, Dkt. Nsubili Mwakapeje alisema kuwa, maandalizi yote ya utoaji chanjo yamekamilika kama serikali ilivyoelekeza ambapo timu za wataalam zipo tayari kuingia katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Siha kuwafikia watoto walengwa.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Siha, Dancan Urrasa alitumia nafasi hiyo kuwasihi Madiwani kutoa ushirikiano kwa wataalam hao wa afya kwa kuwaelimisha wananchi kuwatoa watoto waweze kupatiwa chanjo hiyo.
"Natambua sisi Madiwani ndio tupo karibu na wananchi wetu sasa tushirikiane na wataalam wetu wa afya kuwaelimisha wananchi wetu kutambua umuhimu wa chanjo hii ili waweze kuwatoa watoto wote walengwa wapatiwe chanjo kwa hizi siku nne za kampeni hii" alisema Urrasa.


.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...