Na. Mwandishi Wetu - Nzega

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, leo Agosti 17, 2026, ametembelea, kukagua na kukabidhi miradi inayotekelezwa kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (Agriculture and Fisheries Development Programme – AFDP) katika Shamba la Mbegu la Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA), Kilimi, Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora.

Programu hiyo inafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), ikiwa na lengo la kuongeza tija, kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Kabudi amesema sekta ya kilimo ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake katika pato la Taifa, usalama wa chakula, ajira na biashara ya nje.

“Programu hii ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi ni muhimu kwa sekta ya kilimo kwa kuwa inalenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo ambayo ni mhimili wa maendeleo ya uchumi. Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na ni chanzo cha chakula pamoja na kutoa fursa za ajira kwa zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania,” amesema Prof. Kabudi.

Aidha, Waziri Kabudi amekabidhi rasmi jengo la ofisi, jengo la karakana na jengo la kukaushia mbegu kwa Wizara ya Kilimo, miradi ambayo imetekelezwa kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa ufadhili wa IFAD.

Kabla ya kukabidhi miradi hiyo, Prof. Kabudi alikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Shamba la Mbegu la Kilimi, ikiwemo ujenzi wa karakana, eneo la kukaushia mazao (drying shade), ofisi na ukumbi wa mafunzo pamoja na nyumba mbili za watumishi.

Vilevile, programu hiyo imewezesha upatikanaji wa zana na vifaa vya kisasa vya kilimo, ikiwemo boom sprayer, disc harrow, matrekta, maize sheller, tiller, vifaa vya karakana pamoja na magari kwa ajili ya usimamizi na usambazaji wa mbegu.

Akihitimisha ziara hiyo, Prof. Kabudi amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miradi kwa wakati, kwa kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha iliyowekezwa (value for money) inapatikana.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mpango mkakati madhubuti wa utekelezaji ili kuhakikisha malengo ya Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi yanafikiwa ndani ya muda uliopangwa.

Katika ziara hiyo, Waziri Kabudi ameambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mhandisi Athumani Kilundumya, Mkurugenzi wa Sera na Uratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Paul Sangawe, pamoja na Mratibu wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Salum Mwinjaka.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...