Na: Mwandishi wetu - Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba ameipongeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na
Viatilifu Tanzania (TPHPA) kwa kazi nzuri ya kuhifadhi mbegu za asili na
kupambana na wadudu na magonjwa ya mimea na hivyo kuchangia utoshelevu wa
chakula na kuongeza mapato.
![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru akitoa maelezo kwa waziri Mkuu wakati alipotembelea banda hilo kwenye maonesho wa wakulima Nanenane Jijini Dodoma. |
Pongezi hizo amezitoa wakati
alipotembelea banda TPHPA kabla ya kufungua rasmi maonesho ya wakulima Nanenane
kitaifa Jijini Dodoma na kuelezwa kazi mbalimbali ambazo zinatekelezwa na
mamlaka hiyo zinazoleta tija kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara ya
uuzaji mazao nje ya nchi.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri
mnayoifanya katika kusaidia kutimiza malengo ya Serikali hasa katika eneo la
sekta ya kilimo ambayo inaajiri Watanzania wengi kuliko sekta nyingine yoyote,
endeeeni kuchapa kazi nasi kwa upande wetu kama Serikali tutaendelea kuwaunga
mkono katika kuboresha mazingira ya kazi zenu kwa kuwapatia vifaa na mahitaji
mengine muhimu ili kuongeza tija” alisema Mhe. Nchemba.
Awali akitoa maelezo ya kazi za
Mamlaka hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru
amesema pamoja na majukumu mengi waliyonayo lakini wanasaida kuhakikisha mazao
yanayozalishwa na wakulima nchini yanapimwa ubora wake na kufikia viwango
vinavyohitaji kwenye masoko mbalimbali duniani na hivyo kuingizia taifa fedha
za kigeni.
“Ili makampuni mbalimbali kutoka
Tanzania yaweze kuuza mazao kwenye masoko mbalimbali nje ya nchi kuna vigezo
ambavyo masoko hayo yanahitaji kwenye mazao hayo, hivyo sisi kama mamlaka
tunasaidia kuhakikisha makampuni hayo yanapata bidhaa zenye kukidhi viwango
hivyo na hivyo kuwezesha kufikia soko kulingana na mahitaji ya kila soko na
bidhaa inapouzwa” alieleza Prof. Ndunguru.
Prof. Ndunguru amesema pia jukumu
hilo linakwenda sambamba na kudhibiti visumbufu vya mazao ikiwemo Magonjwa na
wadudu waharibifu wa mazao ili wakulima waweze kulima kilimo chenya tija na
kazi hiyo inafanywa kwa kutumia teknolojia za kisasa kabisa za utambuzi na
udhibiti ikiwemo kipimo cha Vinasaba (DNA) ambacho kinauwezo wa kupima kinasaba
cha kiumbe chochote na kutoa majibu
ndani ya dakika 20.
“Teknolojia hii ya kisasa
tunaenda nayo mahali popote huko kwenye mshamba ya wakulima, tunachukua sampuli
na kupima hapohapo shambani mkulima akiona na ndani ya dakika 20 tunapata
majibu kuwa ni Kirusi gani, Bakteria gani au Fangasi yupi na kupendekeza
kiuatilifu gani au mbinu gani sahihi inafaa kutumika kutatua changamoto
iliyoonekana” alifafanua Mkurugenzi huyo Mkuu wa TPHPA Prof. Ndunguru.
Aidha amesema kuwa kazi nyingine
ambayo TPHPA inafanya ni kutunza nasaba za mimea kwa maana ya Mbegu za asili
zote na mpaka sasa benki hiyo ya mbegu ina aina elfu kumi (10,000)
zimetuzwa kutoka mikoa mbalimbali na za
mazao aina mbalimbali zile za asili kabisa zinazotambuliwa na jamii na zingine
zilikuwa zinaelekea kupotea lakini wamefanikiwa kuzitunza.
Pia Prof. Ndunguru amesema jukumu
lingine muhimu la mamlaka hiyo ni kutoa mafunzo ya matumizi salama ya Viuatilifu
pamoja na kuangalia ubora wa Viuatilifu vilivyopo na vile vinavyoingia nchini
kwa kutumia mitambo na vifaa vya kisasa vilivyopo makao makuu ya TPHPA pale
Arusha na kwenye ofisi za kanda ya mamlaka hiyo ili kusaidia wakulima kupata
viuatilifu salama na kuvitumia kwa usahihi bila kuleta adhari kwao, mazao na
mazingira.
“Kupitia jukumu hilo Mamlaka
imeiongezea Serikali mapato katika mizigo ambayo inasafirishwa kutoka nchini
kwenda nje ya nchi lakini pia kufanikiwa kufungua masoko mbalimbali ya bidhaa
ambayo nchi yetu ilifungiwa kutokana na kutokidhi mahitaji ya masoko yao na
sasa watanzania na makampuni yanauza mazao yetu kwa wingi kwenye masoko hayo
“alifafanua Prof. Ndunguru.
Mamlaka ya Afya ya mimea na
Viuatilifu Tanzania TPHPA inashiriki kwenye maonesho ya wakulima Nanenane
kwenye kanda zote ikiwemo Pwani, Kanda ya kati Dodoma, Kanda ya Kaskazini
jijini Arusha, Kanda ya Kusiki Mbeya na Kanda ya Magharibi Simiyu.
MATUKIO KATIKA PICHA WAZIRI MKUU ALIPOTEMBEA BANDA LA TPHPA KWENYE MAONESHO HAYO.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...