Na Said Mwishehe,Michuzi TV
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la usajili kwa wadau wa uhifadhi na utalii kuwania The Serengeti Awards 2026, huku ikiwasisitiza kutumia fursa hiyo kuonyesha kazi, ubunifu na mafanikio yao katika uhifadhi na uendelezaji wa utalii.
Akizungumza leo Agosti 19,2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk. Thereza Mugobi, amesema dirisha la usajili litafunguliwa Agosti 20, 2026 na kufungwa Septemba 30, 2026, kupitia tovuti rasmi ya tuzo hizo www.serengetiawards.go.tz, ambako wadau watapata taarifa kuhusu kategoria, vigezo na taratibu za kushiriki.
Amefafanua Serengeti Awards zinafanyika kwa mara ya pili ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa wadau katika uhifadhi wa maliasili na urithi wa Taifa pamoja na uendelezaji wa utalii.
“Tuzo hizi zinalenga pia kutoa motisha kwa wadau kuboresha utendaji, kuhamasisha ubunifu na kuongeza ushindani wa Destination Tanzania,” amesema Dk. Mugobi na kuongeza mwaka huu kutakuwa na kategoria 63 katika makundi saba, ambayo ni People’s Choice Awards, Tourism Operator Awards, Tourism Guide Awards, Best Accommodation and Restaurant Services, Conservation Awards, Tourism Exhibitor Awards na Special Appreciation Awards.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Serengeti Awards, Hatibu Madudu, amesema idadi ya kategoria imeongezeka kutoka 56 mwaka jana hadi 63 mwaka huu, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau na kufanya maboresho katika mchakato wa tuzo.
Madudu amesema baadhi ya maboresho yamezingatia changamoto zilizobainika katika mchakato wa mwaka uliopita, huku wananchi wakitarajiwa kushiriki katika mchakato wa kuwapata washindi wa baadhi ya kategoria.
Wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaruhusiwa kuwania tuzo hizo iwapo watatimiza vigezo vilivyowekwa. Serikali imewahakikishia wadau kuwa mchakato wa Serengeti Awards 2026 utasimamiwa kwa kuzingatia uwazi, usawa na uadilifu.



.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...