Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Dodoma imewataka wagonjwa kuwa sehemu ya mchakato wa matibabu kwa kufahamu haki zao na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu afya zao, ikiwa ni pamoja na kupewa taarifa sahihi, kuheshimiwa na kupata huduma salama kwa wakati.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Mgonjwa yaliyofanyika hospitalini hapo leo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk. Abdalah Baja, amesema mgonjwa ana haki ya kupata huduma bora na salama kulingana na mahitaji yake, kushirikishwa katika maamuzi ya matibabu, kupata maoni ya pili ya kitabibu na kuhakikishiwa faragha wakati wa kupatiwa huduma.

Dkte. Baja amesema haki nyingine ni kuheshimiwa utu wa mgonjwa, kulindwa kwa usiri wa taarifa zake za kiafya, kupewa nafasi ya kueleza changamoto zake na kusikilizwa, kuhudumiwa kwa wakati pamoja na kupata taarifa zilizo wazi kuhusu gharama, huduma anazohitaji na maendeleo ya matibabu yake. Dk. Baja alisisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi humwezesha mgonjwa kuelewa huduma anayopewa na kushiriki ipasavyo katika maamuzi ya matibabu.

Pia Dkt. Baja, amesema usalama wa mgonjwa unaweza kuathiriwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika hospitalini katika muda waliopangiwa, kutomuona daktari au kutofanyiwa vipimo walivyoelekezwa, pamoja na changamoto za miundombinu. 

Amesema hali hizo zinaweza kuongeza hatari ya madhara kwa mgonjwa, ikiwamo matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Kwa upande wake, Daktari  bingwa wa Upasuaji toka BMH Kakorongo Mugisha amesema BMH inaendelea kuimarisha usalama wa wagonjwa kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia taratibu za kitaalamu. 

Alisema pia wagonjwa wana haki ya kuamua iwapo wanataka wanafunzi washiriki wakati wa huduma zao, huku hospitali ikiendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kwa kuzingatia ridhaa ya mgonjwa na usalama wake. 

Aidha, alisema muda wa kupata majibu ya vipimo hutegemea aina ya kipimo, ambapo baadhi ya vipimo vya kawaida vinaweza kutoa majibu ndani ya saa tatu, huku vipimo kama CT Scan na MRI vikitarajiwa kutoa majibu ndani ya saa 24 kulingana na taratibu za huduma.

Nao Baadhi ya wagonjwa waliopatiwa huduma BMH wameeleza kuridhishwa na huduma wanazopata, huku wakitoa mapendekezo ya maboresho. Omary Namganda, mkazi wa Kigoma Mjini, aliwapongeza wataalamu wa afya kwa huduma wanazowapatia wagonjwa, wakati Jasery Zacharia wa Kahama, Shinyanga, alisema amepata huduma na ufuatiliaji katika matibabu ya tatizo la figo lililohusisha mawe. Kwa upande wake, Sospiter Chibanila aliitaka hospitali kuendelea kuboresha kasi ya upatikanaji wa majibu ya vipimo vinavyohitaji muda mrefu ili kuwawezesha wagonjwa kupata huduma kwa wakati.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...