Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa uongozi wake mahiri katika kusukuma mbele ajenda ya Afrika ya kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, huku bara hilo likikabiliwa na karibu asilimia 70 ya vifo vya akina mama duniani na takribani theluthi mbili ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano.

Akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, Rais Samia anaongoza ajenda ya “Malengo Matatu ya Sifuri” (Three Zeros) inayolenga kufikia sifuri ya kujifungulia nyumbani, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto mchanga, pamoja na sifuri ya watoto wasiopata chanjo.

Ajenda hiyo imepewa msukumo katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Wakuu wa Nchi kuhusu Afya ya Mama, Mtoto Mchanga na Mtoto, iliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81), ukiwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa taasisi za Umoja wa Afrika, mashirika ya kimataifa ya afya na washirika wa maendeleo.

Akiwasilisha ujumbe wa Rais Samia katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema ukubwa wa changamoto unahitaji Afrika kutoka kwenye ahadi na kuelekea katika hatua madhubuti zinazoweza kupimwa kwa maisha ya wanawake na watoto yanayookolewa.

Amesema, pamoja na hatua ambazo Bara la Afrika limepiga, Afrika bado inachangia karibu asilimia 70 ya vifo vya akina mama duniani na takribani theluthi mbili ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano, huku sehemu kubwa ya vifo hivyo ikiwa inaweza kuzuilika.

Makamu wa Rais amesema msukumo wa Rais Samia unalenga kuimarisha mifumo ya afya ya nchi za Afrika, kuongeza ufadhili wa ndani, kuboresha huduma za dharura na mifumo ya rufaa, kuongeza upatikanaji wa wahudumu wa afya wenye ujuzi na kuhakikisha takwimu zinatumika kufuatilia matokeo na kubaini maeneo yanayohitaji hatua zaidi.

Akielezea uzoefu wa Tanzania, Makamu wa Rais amesema uwekezaji katika huduma za afya ya msingi na za dharura kwa mama na mtoto mchanga, pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya rufaa ikiwemo M-Mama, unaonesha namna uongozi wa kisiasa, teknolojia na utoaji wa huduma kwa wananchi vinavyoweza kuunganishwa katika kuokoa maisha.

Hatua hizo zimekwenda sambamba na kuongezeka kwa wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022, mafanikio yanayoonesha uwezekano wa kubadili mwenendo wa vifo vya mama na mtoto pale uwekezaji unapounganishwa na utekelezaji katika ngazi ya jamii.

Makamu wa Rais alisema ajenda anayoiongoza Rais Samia pia inatoa uzito kwa suala la Afrika kujitegemea katika afya, akisisitiza kuwa mafanikio hayapaswi kupimwa pekee kwa uwezo wa bara kugharamia, kuzalisha au kununua mahitaji yake, bali pia kwa uwezo wa kuhakikisha huduma muhimu zinamfikia kila mama na mtoto kwa wakati na mahali wanapozihitaji.

Katika kufanikisha hilo, nchi za Afrika zimehimizwa kuimarisha uwajibikaji wa kisiasa, kuongeza uwekezaji wa ndani katika huduma zinazookoa maisha na kuhakikisha rasilimali zinafika hadi katika ngazi ya utoaji huduma.

“Dhamira ni kuhakikisha hakuna mama anayepoteza maisha kwa kukosa usafiri, damu, mhudumu mwenye ujuzi au huduma ya dharura; hakuna mtoto mchanga anayefariki kwa kukosa huduma inayoweza kuokoa maisha yake, na hakuna mtoto anayebaki bila chanjo kwa sababu mfumo wa afya haukuweza kuifikia familia yake,” amesema Mhe. Ndejembi.

Makamu wa Rais amesema kulinda uhai wa mama na mtoto si suala la afya pekee, bali ni uwekezaji katika rasilimali watu, uchumi na mustakabali wa Afrika, pamoja na kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Bara la Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dkt. Jean Kaseya, alipongeza uongozi wa Rais Samia na kueleza dhamira ya Taasisi hiyo kuendelea kumuunga mkono katika jukumu lake la Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, huku akitaja hatua zilizopigwa na Tanzania kama mfano wa mafanikio yanayoweza kupatikana barani Afrika.

Takwimu za Africa CDC zinaonesha kuwa Tanzania imepunguza uwiano wa vifo vya uzazi kwa takribani asilimia 80, kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022, hatua inayohusishwa na kuimarishwa kwa huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga, mifumo ya rufaa, ongezeko la wahudumu wa afya pamoja na ufuatiliaji wa vifo vya mama na watoto.

Dkt. Kaseya alisema Africa CDC itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kusukuma mbele ajenda hiyo, akisisitiza umuhimu wa uongozi wa kisiasa, uwekezaji na mifumo imara ya afya katika kulinda uhai na ustawi wa mama na mtoto barani Afrika.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Adhanom Ghebreyesus amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuandaa mkutano huo na kuwa kinara wa Umoja wa Mataifa wa Afya ya Mama na Mtoto. Amesema katika kipindi cha miaka sita pekee, Tanzania imepunguza kiwango cha vifo vya kina mama kwa asilimia 81. Amesema kwa kuzindua mpango mkakati huo wa sifuri tatu (Three Zeros), Tanzania inaongoza kwa mfano na inapaswa kuungwa mkono.

Amesema Shirika la Afya Duniani limejidhatiti kusaidia kila nchi mwanachama kulingana na mazingira yake na kufikia malengo yake kwa kuimarisha viwango vya huduma za kitabibu vinavyotumiwa na wahudumu walio mstari wa mbele kuokoa maisha ya kina mama na watoto wachanga.

Kupitia nafasi yake kama Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, Rais Samia anasukuma dhamira ya kulifanya bara hilo kufikia hatua ambayo vifo vinavyoweza kuzuilika havitachukuliwa tena kuwa jambo lisiloepukika, huku kaulimbiu ya “Jiongeze, Tuwavushe Salama” ikibeba wito wa Afrika kwenda hatua ya ziada kwa ajili ya kila mama, mtoto mchanga, mtoto na kijana balehe.

Mkutano huo, umehudhuriwa na Viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dkt. Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) Dkt. Jean Kaseya, Mwenza wa Rais wa Benin Bi. Nathalie Vilette Wadagni, Wadau wa Maendeleo wakiwemo, Gates Foundation, Global Fund, Gavi, UNFPA, Unicef, Suzan Thompson Buffett Foundation, Beginning Fund pamoja na Viongozi kutoka Umoja wa Afrika (AU).





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...