Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimeridhishwa na uhai wa chama na utekelezaji wa shughuli zake katika Mkoa wa Tanga, kikieleza kuwa ushirikiano mzuri kati ya chama na Serikali umewezesha kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, wakati akiendelea na ziara mkoani Tanga yenye lengo la kukagua uhai wa chama pamoja na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.
Kihongosi amesema miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Mkinga ni upatikanaji wa maji, akieleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga Sh35 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji katika eneo hilo.
“Changamoto kubwa inayowakabili wananchi hapa ni suala la maji, lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta Sh35 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji,” amesema Kihongosi.
Kihongosi ameyasema hayo leo Septemba 25,2026 wakati akizindua Shina Namba 6 lililopo Mbuyuni, Kata ya Manza, ambapo amesema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za maji, afya na elimu.
Amesema Serikali inayoongozwa na CCM chini ya Rais Samia imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi na wananchi wanapata huduma muhimu pamoja na mazingira bora ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya CCM na Serikali ni muhimu katika kuhakikisha ilani ya chama inatekelezwa na ahadi zinazotolewa kwa wananchi zinatimizwa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...