Na George Maziku, Mbogwe

CHANZO cha mgogoro baina ya mgodi wa INK na Mayombya Gold Mine iliyopo kata ya Lugunga, wilayani Mbogwe, mkoa wa Geita, kimewekwa hadharani.

Mgogoro huo umesababisha Serikali kuifunga migodi hiyo kwa muda mwisho wa wiki iliyopita ili kupisha uchunguzi, unadaiwa kuchochewa na kampuni ya Dwasi Simon Company Limited, inayomiliki duara namba F1 iliyopo ndani ya leseni ya Mayombya Gold Mine.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mgogoro huo, Meneja Mkuu wa mgodi wa Mayombya Gold Mine Majuto Manyilizu alisema uongozi wa mgodi wake hauwatambui wachimbaji wa kigeni kutoka China, bali unamtambua na umeingia mkataba na mwekezaji mtanzania aitwaye Dwasi Simon Company Limited anaemiliki duara namba F1.

“Kwenye leseni yangu sina wachimbaji wachina, siwatambui wala sijaingia mkataba na wachina,nimeingia mkataba na mwekezaji anayeitwa Dwasi Simon Company Limited ambaye anamiliki duara namba F1, huyu ndiye ninamtambua kama mwekezaji kwenye leseni yangu”, alifafanua Manyilizu.

Hata hivyo, Manyilizu alikiri kufahamu uwepo wa raia hao wa kigeni kutoka China, wanaofanya kazi ya uchimbaji kwenye kitalu kinachomilikiwa na Dwasi Simon Company Limited.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo mgogoro baina ya migodi hiyo miwili inayohusu kuingiliana kwa mipaka pamoja na matumizi ya milipuko mikubwa inaayodaiwa kufanywa na mgodi wa Mayombya ambayo inaathiri shughuli za uchimbaji katika mgodi wa INK.

Mgogoro huo ulichukua sura mpya Ijumaa, wiki iliyopita, baada ya uamuzi wa Tume ya Madini nchini kusitisha shughuli za uchimbaji katika migodi yote miwili ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na wataalamu wa tume hiyo.

Kiini cha mgogoro huo kinadaiwa kuwa ni vitendo vya wachimbaji wa kichina kuendesha shughuli za uchimbaji bila kuzingatia kwanza mipaka baina ya mgodi wa Mayombya na mgodi jirani wa INK, ambapo inadaiwa wamevuka mpaka na kuingia eneo la leseni la mgodi wa INK.

“Mojawapo ya changamoto zilizozalisha mgogoro huu ni shughuli za kichimbaji za daraja la kati zinazoendeshwa katika leseni ya jirani zetu kwa kutumia raia wa kigeni ambazo zinaambatana na milipuko mikubwa ambayo zimeleta athari kubwa katika maduara yanayomilikiwa na wachimbaji wadogo kwenye mgodi wetu…

“Uchunguzi wa awali unaashiria hatari kubwa kama hatua za haraka hazitachukuliwa kunaweza kutokea ajali kubwa na kusababisha mauaji ya wachimbaji wengi”, alisisitiza Meneja Mkuu wa mgodi wa INK Farid Lugwisha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Dwasi Simon Company Limited , Dwasi Simon alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa mgogoro huo hakuwa tayari kuzungumza kwa madai alikuwa msibani wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, hivyo akimtaka mwandishi kusubiri hadi atakaporejea Mbogwe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...