Na Mwandishi Wetu
BOHARI ya Dawa (MSD) imefanikiwa kuingiza nchini shehena ya kwanza ya dawa ya Naltrexone, inayotumika katika matibabu ya uraibu wa pombe.
Hatua hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya MSD na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, katika kuimarisha huduma za matibabu ya uraibu wa pombe nchini.
Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa MSD, Etty Kusiluka, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa makubaliano ya kuimarisha huduma kati ya MSD na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, hususan katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za kudhibiti uraibu wa pombe.
“Dawa ya Naltrexone itapatikana na kuratibiwa na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, huku ikiwa ni bidhaa itakayoendelea kununuliwa na MSD kwa ajili ya taasisi hiyo,” amesema.
Amesema mapema mwezi huu, wakati wa mafunzo kuhusu matumizi ya dawa hiyo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, aliiagiza MSD kuharakisha upatikanaji wa vidonge hivyo.
Kusiluka ameongeza kuwa kupokelewa na kuingizwa nchini kwa shehena hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya ya akili na tiba ya uraibu wa pombe.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha juhudi za Serikali kupitia MSD na wadau wa sekta ya afya kuhakikisha bidhaa muhimu na za kimkakati za afya zinapatikana nchini kwa wakati.


.jpeg)

.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...