Na Said Mwishehe,Michuzi TV


MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Edward Mpogolo, amesema wilaya hiyo inaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu uondoaji wa taka na usafi wa mazingira huku akisisitiza suala la usafi ni wa kila siku.

Pia amesema viongozi, wananchi, wafanyabiashara na viongozi wa masoko wameendelea kushirikiana kuhakikisha maeneo mbalimbali yanakuwa safi, hususan katika masoko makubwa yaliyopo wilayani Ilala.

Mpogolo ameyasema hayo leo Septemba 5,2026 wakati aliposhiriki usafi katika Soko la Buguruni akiungana na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya, viongozi, wafanyabiashara na wananchi.

Amesema katika Wilaya ya Ilala kuna masoko makubwa yakiwemo Soko la Samaki Feri, Soko la Kisutu, Soko la Buguruni na Soko la Ilala, akisisitiza kuwa usafi katika maeneo hayo ni jukumu la kila mmoja.

“Kama unavyojua Ilala ndiyo tuna masoko makubwa, hivyo nitumie nafasi hii pia kuwaelekeza viongozi wa masoko na wafanyabiashara kuhakikisha wanafanya usafi na kuyaweka masoko yao katika hali ya usafi,” amesema Mpogolo.

Ameongeza hatua zilizochukuliwa na wafanyabiashara zimeanza kuonekana, ambapo baadhi yao wamejitokeza kufanya usafi katika maeneo yao ya biashara na wengine wameondoa bidhaa zilizokuwa zimepangwa barabarani na kuzipeleka ndani ya masoko.

“Leo hii ninyi ni mashahidi, mmeona wafanyabiashara walioko mbele ya Soko la Buguruni ambao waliopanga barabarani wameondoa bidhaa zao kwa sababu wanatambua pia na wao walikuwa wanafanya makosa kufanyia biashara zao maeneo ya barabara,” amesema.

Mpogolo pia amewashukuru wananchi na wafanyabiashara wote waliojitokeza kushiriki katika zoezi la usafi, akisema Jiji la Dar es Salaam limeweka utaratibu wa kuhakikisha usafi unafanyika kila siku.

Amesema hatua hiyo inalenga kulirejesha jiji katika hali nzuri ya usafi na kulifikisha katika kiwango kinachoridhisha, sambamba na kutekeleza maelekezo ya Rais.

“Tumeshakubaliana kwamba tutahakikisha tunafanya usafi kila siku katika Jiji la Dar es Salaam ili lifike katika standard ambayo inaridhisha kama Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alivyotuelekeza.Kwa sasa usafi kwa Dar es Salaam ni kila siku,” amesema.

Aidha, amewataka wananchi wote wa Ilala kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake katika kutunza usafi kwenye maeneo yao ya biashara na makazi.

Pamoja na hilo, amewataka wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao barabarani kuondoa bidhaa hizo, akieleza kuwa maeneo hayo yamewekewa miundombinu maalumu kwa ajili ya watembea kwa miguu.

Mpogolo amesema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ameelekeza magari ya matangazo kwenda katika maeneo mbalimbali kutoa elimu na tahadhari kwa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao barabarani ili waondoe.

“Katika barabara zile nimewekwa pavement, wako wapita kwa miguu ambao wanatakiwa kupita kwenye maeneo yale, lakini magari yanatakiwa kuendelea kupita vizuri,hivyo hatutarajii wafanyabiashara kupanga bidhaa zao barabarani.”

Amesisitiza usafi na matumizi sahihi ya maeneo ya umma ni wajibu wa kila mwananchi ili kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi, salama na lenye mazingira bora kwa shughuli za kila siku.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...