-Awapa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na wakurugenzi wa halmashauri
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Yusufu Masauni ametoa mwito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuweka utaratibu kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku ya usafi wa Mazingira Kitaifa.
Ametoa mwito huo leo Septemba 5,2026 aliposhiriki ufanyaji usafi katika Soko la Buguruni Jijini Dar es Salaam, Septemba 5, 2026 ambapo amefafanua Serikali kupitia Rais Dk.Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais mwaka 2016 alitoa agizo kuwa kila Jumamosi ya mwisho ya mwezi kuwa siku ya usafi wa Mazingira Kitaifa.
Aidha amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa ‘Enviromental Management (Designation of National Cleanliness Day) Guidelines , 2016,chini ya G.N.No.139. Mwongozo huo unaelekeza utekelezaji wa tamko la Serikali la kuitangaza kila jumamosi ya mwisho wa Mwezi kuwa siku ya usafi wa Mazingira Kitaifa.
Mhandisi Masauni amesema kwa muktadha huo, Serikali inatoa mwito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu wa kusimamia utekelezaji wa maelekezo haya kwa kuzingatia maslahi ya makundi mbalimbali.
Amesisitiza ni wajibu wa kila mwananchi, mfanyabiashara, mwekezaji, taasisi za Serikali, sekta binafsi, viongozi wa mitaa, wenye viwanda, watoa huduma za taka, taasisi za elimu na jamii kwa ujumla kuwa na utaratibu wa kufanya na kusimamia Usafi wa Mazingira katika maeneo yao.
“Hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila Mtanzania kushiriki katika usafi wa mazingira.” Amesema Mhe. Masauni.Taka zinapotupwa hovyo, mifereji inapoziba, maeneo ya biashara yanapokuwa machafu au taka ngumu na hatarishi zinaposhughulikiwa bila utaratibu, madhara yake huonekana katika afya ya wananchi, miundombinu, mito, bahari na uchumi.”
Waziri Masauni amesema Mazingira machafu yanaweza kuchangia kuenea kwa magonjwa, kuongeza gharama za usafi na afya, kupunguza mvuto wa miji yetu kwa watalii na wawekezaji, na kuharibu rasilimali ambazo Watanzania wanategemea kwa maisha yao.
Pia amesema usimamizi wa taka hususan katika maeneo ya mjini hairidhishi ambapo wastani wa asilimia 37 tu ya taka ngumu zinazozalishwa hukusanywa na hivyo kiasi kikubwa cha taka huzagaa.
Kwa upande mwingine amesema, taka zinaweza kuwa fursa ya kiuchumi kupitia urejelezaji uchumi rejeshi, taka kutumika kama chanzo cha uzalishaji wa Nishati, Uzalishaji wa mbolea (mboji) na biashara ya kaboni.
Mathalani, Tanzania ina fursa ya uwekezaji wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 22 kutoka katika taka plastiki, karatasi chakavu, taka za kielektroniki na betri chakavu.
Pamoja na hayo amewakumbusha kuwa Serikali ilishazuia matumizi ya mifuko ya plastiki kutokana na athari za kimazingira na ilishakaa kikao na wazalishaji wa mifuko hiyo kutengeneza mifuko ambayo ni rafiki wa mazingira ili wafanyabiashara watumie mifuko hiyo.
“Nimeona bado mifuko ya plastiki inatumiwa na baadhi ya wafanyabiashara,nawakumbusha mifuko ya plastiki tulishaizuia hivyo wanaotengeneza mifuko tunawakumbusha kuwa na mifuko mbadala badala ya kutengeneza mifuko ya plastiki.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...