Na Mwandishi Wetu

MTAALAMU katika sekta ya nishati, hususan mafuta nchini, Dkt. Sajad Habib Rai, ameteuliwa kuwa mjumbe na mmoja wa wazungumzaji katika Mkutano wa World CEO Summit 2026 Africa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 26 na 27, 2026, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa kimkakati unaolenga kujadili masuala ya uwekezaji, biashara na maendeleo ya kiuchumi, unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya Wakurugenzi Wakuu (CEOs) 1,000, wawekezaji, watunga sera na viongozi wa sekta mbalimbali kutoka zaidi ya nchi 50.

Dkt. Sajad, ambaye ni Meneja Mkazi wa Mansoor Industries Limited, anatarajiwa kuzungumzia uzoefu wake katika masuala ya maendeleo ya viwanda, nishati, uwekezaji, uendelevu na ushirikiano wa kimkakati kwa ajili ya kukuza uchumi wa Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji wa mkutano huo, Dkt. Rai atashirikisha mitazamo na uzoefu kuhusu maendeleo ya viwanda, nishati, uendelevu na uwekezaji, pamoja na ushirikiano wa kimkakati unaohitajika kuimarisha uwezo wa uzalishaji barani Afrika na kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi.

Akizungumzia ushiriki wake katika mkutano huo, Dkt. Sajad, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mshauri katika sekta ya nishati, hususan mafuta, amesema anatarajia kutumia fursa hiyo kushirikisha uzoefu wake na kujifunza kutoka kwa wazungumzaji na washiriki wengine.

“Nimepokea mwaliko wa mkutano huo kwa furaha kubwa. Lengo ni kuchangia uchumi wa nchi yetu na kuhamasisha uwekezaji. Hivyo, nami kama mzalendo wa nchi hii nitajifunza mengi, lakini pia nitatoa uzoefu wangu ili kwa pamoja tuweze kuijenga Tanzania na Afrika inayojitegemea kiuchumi,” amesema Dkt. Sajad.

Amesema ushiriki wake katika mkutano huo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania katika jukwaa la kimataifa, hususan katika maeneo ya uwekezaji, nishati na maendeleo ya viwanda.

World CEO Summit Africa ni mkutano unaowakutanisha viongozi wa kampuni, Serikali na wawekezaji kwa lengo la kujadili namna ya kukuza biashara na uchumi wa Afrika.

Mkutano wa mwaka huu una kaulimbiu isemayo “Uniting Leadership, Capital and Policy for Africa’s Transformation”, inayolenga kuunganisha uongozi, mitaji na sera kwa ajili ya kuharakisha mabadiliko ya Afrika.

Miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni upatikanaji wa mitaji, maendeleo ya viwanda na biashara, uongozi na sera za kiuchumi, teknolojia na ubunifu wa Akili Unde (AI), nishati na miundombinu, pamoja na kilimo na usalama wa chakula.

Masuala mengine ni huduma za kifedha, afya na mali isiyohamishika, uendelevu na ukuaji wa biashara, pamoja na ushirikiano wa kimkakati, ubia na upanuzi wa masoko.



Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...