Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mtu atakayebainika kutupa taka hovyo jijini Dar es Salaam atatozwa faini ya Shilingi 300,000 hadi milioni moja au kuhukumiwa kifungo cha miezi 12 hadi 24, kwa mujibu wa Kifungu cha 41 cha Sheria Ndogo ya Afya, Usafi na Usimamizi wa Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ya Mwaka 2024 (GN Na. 1011).

Akizungumza jana, Septemba 19, 2026, baada ya kuhitimisha zoezi la usafi wa mazingira jijini, Mpogolo amesema sheria hiyo imeanza kutekelezwa kikamilifu kwa lengo la kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa safi, salama na yenye mazingira bora.

“Atakayekutwa anatupa uchafu hovyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Adhabu ni faini ya kuanzia Shilingi laki tatu hadi milioni moja au kifungo cha miezi 12 hadi 24. Kila mmoja anatakiwa kutambua wajibu wake na kuacha mara moja tabia ya kutupa uchafu hovyo,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira, lakini hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka sheria kwa kutupa taka hovyo, kutiririsha maji au kufanya vitendo vingine vinavyohatarisha usafi na mazingira.

Mpogolo amesema utekelezaji wa sheria hiyo haulengi kutoa adhabu pekee, bali kujenga nidhamu, uwajibikaji na utamaduni wa usafi miongoni mwa wananchi.

Amesema Halmashauri itaendelea kuweka maeneo na vifaa vya kuhifadhia taka pamoja na kuhamasisha utenganishaji wa taka kulingana na aina zake ili kurahisisha ukusanyaji na utunzaji wa mazingira.

Ili kuimarisha ufuatiliaji, Mpogolo amesema Jiji limejipanga kuajiri vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kuwapatia vyombo vya usafiri kwa ajili ya kusimamia usafi katika mitaa mbalimbali.

“Tutakwenda mtaa kwa mtaa. Hatutaki kuona mtu anatupa taka popote anapotaka. Tutakuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha sheria inatekelezwa ipasavyo,” amesema.

Aidha, amesema barabara zote muhimu za Jiji, maarufu kama Smart Roads, zitasimamiwa kikamilifu ili zibaki safi, zipandwe miti rafiki na salama na ziendelee kulipamba Jiji.

Amesema biashara katika barabara hizo hazitaruhusiwa bila kibali cha Mkurugenzi wa Jiji, huku wafanyabiashara wakitakiwa kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyopangwa.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano, kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara na kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa na mazingira safi na yanayovutia.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...