Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetoa elimu kuhusu tahadhari za majanga ya asili, masuala ya jiolojia na El Nino kwa wakazi wa Kijiji cha Mamba Miamba, Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Elimu hiyo imetolewa leo katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa Serikali ya Kijiji, Mtendaji wa Kijiji pamoja na wananchi, ambapo wamejadili hatua mbalimbali za kuchukua ili kupunguza athari za majanga ya asili katika eneo hilo.

Kikao hicho kimefanyika kufuatia ombi la Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, alilolitoa Septemba 28, 2026, baada ya semina iliyowakutanisha maafisa tarafa, madiwani na watendaji wa kata.

Katika semina hiyo, pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo hatarishi yaliyopo upande wa tambarare, mbunge huyo aliwaomba wataalamu kufika maeneo ya milimani kwa ajili ya kutoa elimu na ushauri wa kitaalamu kwa wananchi.

Katika kikao hicho, wananchi wamekubaliana kusitisha mara moja shughuli za kilimo katika eneo lililowahi kuathiriwa na maporomoko ya udongo mwaka 2009.

Badala yake, wamekubaliana kupanda miti katika eneo hilo ili kusaidia kurejesha uimara wa udongo na kupunguza mmomonyoko.

Aidha, wananchi wameiomba Serikali kuchukua hatua za kudhibiti athari za radi katika eneo hilo, ikiwemo kuweka mifumo au vifaa maalumu vya kinga dhidi ya radi, kutokana na eneo hilo kuwa na historia ya kukumbwa na matukio ya radi mara kwa mara.

Wataalamu wa GST wamewasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya asili, pamoja na kuchukua hatua mapema wanapoona dalili zinazoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali.

GST imeendelea kutoa elimu kwa jamii katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu masuala ya jiolojia, majanga ya asili na namna ya kuchukua tahadhari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi na kupunguza athari za majanga yanayoweza kujitokeza.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...