Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SHAHIDI wa tano wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, John Heche, ameieleza Mahakama namna matukio mbalimbali aliyodai kuyashuhudia katika chaguzi yalivyosababisha chama hicho kufikia msimamo wa “No Reforms, No Election” (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi).
Heche, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, ametoa ushahidi huo leo Septemba 9, 2026, katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dustun Ndunguru.
Akijibu maswali ya Lissu, Heche amesema Desemba 2, 2024, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikaa na kujadili masuala mbalimbali yaliyohusu chaguzi, ikiwemo ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, kuenguliwa kwa wagombea wa chama hicho na matukio ya mauaji yaliyohusishwa na chaguzi.
Heche amesema kutokana na hali hiyo, hususani uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na chaguzi nyingine alizoshiriki na kuzishuhudia, chama hicho kiliona kuwa hazikuwa chaguzi za kawaida bali “uchafuzi”, jambo lililopelekea Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wa wakati huo, Freeman Mbowe, kufikia msimamo wa “No Reforms, No Election.”
Amesema mabadiliko yaliyokuwa yakihitajika yalihusisha marekebisho makubwa ya Katiba na sheria, pamoja na kuondoa madaraka makubwa ya Rais katika uundaji wa Tume ya Uchaguzi na uteuzi wa watendaji wa uchaguzi.
“Kamati Kuu iliazimia mabadiliko makubwa ya kikatiba na ya kisheria,” amesema Heche.
Amedai chama hicho kilitaka Tume Huru ya Uchaguzi ambayo ingekuwa huru na isiyo na upendeleo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine.
Heche amesema Aprili 3, 2025, CHADEMA ilikutana na watia nia waliokuwa wakitarajia kugombea kupitia chama hicho katika makao makuu ya chama, Mikocheni, Dar es Salaam, na kuwaeleza sababu za kuendelea na msimamo wa “No Reforms, No Election” uliokuwa umechukuliwa tangu Desemba 2024.
Akieleza matukio aliyodai kuyashuhudia katika chaguzi mbalimbali, Heche amesema ameshiriki chaguzi akiwa mgombea na kiongozi wa chama, ikiwemo uchaguzi wa Arumeru, Busanda, Igunga, Kinondoni pamoja na chaguzi za mwaka 2015 na 2020.
Amedai chaguzi hizo ziliambatana na matukio mbalimbali, ikiwemo mauaji ya wanachama, kuenguliwa kwa wagombea wa CHADEMA, kunyimwa fomu za viapo vya mawakala, mawakala kuondolewa vituoni wakati zoezi likiendelea, polisi kupiga watu na kuvuruga mikutano ya kampeni ya chama hicho.
Amedai pia kuwa wagombea wa chama hicho walinyimwa fomu za matokeo, huku akidai kulikuwa na kura za uongo kuingizwa na baadhi ya watu kubeba vibegi vya kura feki.
Akijibu maswali ya Lissu kuhusu matukio ya mauaji aliyoyakumbuka katika chaguzi hizo, Heche ameeleza tukio la uchaguzi wa mwaka 2015 katika Jimbo la Busanda, ambapo amesema kiongozi wa CHADEMA na mgombea wa ubunge, Alphonce Mawazo, aliuawa.
Amesema Mawazo alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita na Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho.
Alipoulizwa kama kuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika na mauaji ya Mawazo, Heche amesema hakumbuki vizuri mwisho wa kesi hiyo hivyo hawezi kueleza kwa usahihi.
Katika tukio lingine, Heche amesema wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020, alipokuwa akifunga kampeni Nyamongo, Kata ya Matongo, alivamiwa na kushambuliwa kwa risasi, ambapo watu wawili waliuawa na wengine kujeruhiwa.
Lissu pia amemuuliza Heche kuhusu tukio jingine la mauaji katika jimbo lake.
Heche amesema polisi walimuua mdogo wake, Suguta Heche, ambaye alidai alikuwa amefungwa pingu mikono yote na kuchomwa kisu.
Alipoulizwa kuhusu hatua zilizochukuliwa, Heche amesema Kamanda wa Polisi wa wakati huo alitoa taarifa kuthibitisha kuwa Suguta aliuawa na polisi na kwamba hatua zingechukuliwa dhidi ya waliohusika.
Hata hivyo, amesema polisi huyo aliachiwa na mpaka sasa ni mtumishi wa Jeshi la Polisi.
Ushahidi huo umetolewa wakati Heche akiendelea kujibu maswali ya Lissu katika hatua ya utetezi wa kesi hiyo.
Shauri hilo limeahirishwa hadi kesho, ambapo Heche ataendelea kutoa ushahidi wake, huku Majaji wakitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu mashahidi wengine waliowekewa pingamizi.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...