Bodi ya Wakurugenzi ya INADES Formation Tanzania imefanya kikao chake cha kwanza tangu ichaguliwe mwezi Mei, kikilenga kupitia utekelezaji wa bajeti na shughuli za taasisi kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026, pamoja na kujadili mipango ya utekelezaji kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2026.

Akizungumza Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Alphonce Katunzi, Jijini Dodoma, amesema lengo ni kuhakikisha kuwa mipango ya taasisi inaendana na mahitaji halisi na kwamba rasilimali zilizopo zinatumika kwa ufanisi katika kutekeleza majukumu na kufikia matokeo yaliyokusudiwa.

Amesema taasisi hiyo inataka kuendelea kuboresha namna inavyotekeleza shughuli zake, ikiwemo kuhakikisha huduma na programu zinazotolewa zinaendana na mahitaji ya jamii na wanufaika, kwa kuzingatia mfumo unaoangalia mahitaji halisi.

Amesema kikao hicho pia kimejadili na kupitisha makadirio ya bajeti ya mwaka 2027, huku kikifanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026 kwa kipindi cha Januari hadi Juni na kuangalia mipango ya utekelezaji kwa kipindi kilichobaki cha mwaka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa INADES Formation Tanzania, Jacquline Nicodemas, amesema kabla ya kikao cha bodi, kwa takribani siku tatu kulifanyika vikao vya kiutendaji na kimaamuzi, ikiwemo vya Kamati ya Fedha, Rasilimali Watu na Utendaji Kazi pamoja na Kamati ya Mafunzo na Afya ya Jumuiya.

Amesema vikao hivyo ni sehemu ya kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na utendaji wa taasisi, huku akieleza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni taasisi imetekeleza programu kuu mbili zilizosaidia kuimarisha ushirikiano na Serikali, wadau mbalimbali pamoja na jamii, ikiwemo kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Specioza Kifuto, amesema baada ya kikao hicho wanatarajia wanajumuiya na wadau kuanza kuona mabadiliko katika utekelezaji wa shughuli za taasisi, ikiwemo kuboreshwa kwa huduma zinazotolewa kwa wakulima na jamii kwa ujumla, amesisitiza wadau kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli, kutumia mafunzo wanayopata katika vitendo na kushiriki katika kutekeleza maamuzi yaliyokubaliwa.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...