Kamati ya Mawaziri cha Jumuiya ya Madola wanaosimamia Utekelezaji wa Maadili (CMAG) imetambua na kufurahishwa na ushirikiano mzuri ulioonyeshwa na serikali ya Tanzania pamoja na hatua zilizochukuliwa kuwezesha maridhiano huko Zanzibar.

Kamati hiyo katika kikao chake cha 74 imesema hatua hizo zilizochukuliwa ni msingi thabiti wa maendeleo zaidi ya kidemokrasia na kisiasa nchini Tanzania.

Kikao hicho maalum kiliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ulaya wa Malta, Mheshimiwa Chris Fearne.

Katika kikao hicho kilichofanyika mjini New York, viongozi na wawakilishi mbalimbali wa ngazi za juu walihudhuria, wakiwemo Naibu Waziri Mkuu wa Samoa, Mheshimiwa Mulipola Anarosa Ale Molioʻo, pamoja na mawaziri na wawakilishi maalum kutoka nchi wanachama wa Antigua na Barbuda, Botswana, Canada, Grenada, Malaysia, Mauritius, na Zambia.

Uwepo wa viongozi hawa ulitoa fursa ya kufanya tathmini ya kina kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu nchi wanachama, ikiwemo Tanzania na Uganda, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora, na ushirikiano ndani ya familia ya Jumuiya ya Madola.

Katika taarifa iliyotolewa kufuatia kikao chao maalum kilichofanyika pembezoni mwa Mkuu wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, pamoja na kutambua maendeleo hayo chanya katika maeneo mbalimbali, CMAG ilisisitiza haja ya kuendelea kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha kunakuwa na mchakato jumuishi na wa wazi wa mazungumzo ya kisiasa ya vyama vingi, sambamba na kulinda kwa dhati uhuru wa kiraia, kisiasa, na vyombo vya habari.

Kabla ya taarifa kamati hiyo ili ilipokea taarifa iliyowasilishwa kwa kina na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Palamagamba Kabudi.

CMAG imesifu utayari wa nchi ya Tanzania kushirikiana na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo katika kuimarisha misingi ya maridhiano na maelewano ya kitaifa.

Hata hivyo walitilia mkazo maalum katika umuhimu wa kuzingatia taratibu za kisheria zilizo wazi, za haki na kwa wakati unaofaa katika mashauri yote yaliyopo wazi, pamoja na kuweka michakato inayoaminika ya uwajibikaji, utoaji wa haki na fidia stahiki kwa wale wote waliothiriwa na matukio mbalimbali ya nyuma, ili kuimarisha zaidi uaminifu na ustawi wa jamii.

Kufuatia tathmini hiyo ya kina, Jumuiya ya Madola imeihimiza serikali ya Tanzania kupanga tarehe ya mapema kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ili apate fursa ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine muhimu wa maendeleo na siasa nchini.

Kutokana na umuhimu wa mazungumzo hayo na hatua zinazoendelea kuchukuliwa, kikao hicho kiliafikia makubaliano ya kuendelea kuweka Tanzania kwenye ajenda yake rasmi ya ufuatiliaji, huku wakithibitisha utayari wa kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu na serikali katika kuhakikisha malengo ya kidemokrasia, amani, na maendeleo endelevu yanatimizwa kwa maslahi mapana ya wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kamati hiyo ya Mawaziri cha Jumuiya ya Madola inayosimamia Utekelezaji wa Maadili (CMAG) ilianzishwa mwaka 1995 ili kuwa mlinzi na mtetezi wa maadili na misingi ya kisiasa ya Jumuiya ya Madola.

Kamati hiyo inaundwa na mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama nane zinazozunguka kanda mbalimbali kwa mfumo wa zamu, ikijumuisha pia waziri wa mambo ya nje wa nchi iliyo Mwenyekiti Mkuu wa sasa wa Jumuiya hiyo ambaye ni mwenyeji wa Mkutano uliopita wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).

Kikao hicho cha 74 kiliitishwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mheshimiwa Shirley Botchwey.


Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...