Na Farida Said Mkinga Tanga

Uwekezaji mkubwa unaotekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe kupitia ujenzi wa Kampasi ya Tanga, iliyopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, unatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kielimu, kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Kampasi hiyo inatarajiwa kufungua fursa mbalimbali kwa wananchi wa Mkinga na maeneo jirani, ikiwemo upatikanaji wa elimu ya juu, huduma za afya, ajira, biashara pamoja na kuvutia uwekezaji katika maeneo mbalimbali.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, alipofanya ziara katika eneo la ujenzi wa Kampasi hiyo lililopo Kata ya Gombero, Wilaya ya Mkinga.

Ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya ujenzi wa Kampasi hiyo pamoja na kusisitiza umuhimu wa kukamilisha miundombinu iliyosalia ili Kampasi hiyo ianze kutoa huduma zilizokusudiwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Shein amesema uwekezaji huo ni sehemu ya maono ya muda mrefu yenye manufaa mapana kwa jamii, akibainisha kuwa ubora wa majengo na miundombinu unaoonekana katika eneo hilo unaonesha dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kujenga miundombinu endelevu itakayohudumia vizazi mbalimbali.

“Tunachokijenga hapa si kwa ajili yetu tu. Watakaokuja kunufaika zaidi ni watoto wetu, wajukuu zetu na vizazi vinavyofuata,” amesema Dkt. Shein.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema Kampasi hiyo ipo katika hatua za mwisho kuelekea kuanza kutoa huduma.

Amesema kazi kubwa iliyosalia ni ukamilishaji wa maeneo mbalimbali ya Kampasi, ambapo mkandarasi anaendelea na kazi hizo kabla ya miundombinu hiyo kuwa tayari kwa matumizi.

Kwa mujibu wa Prof. Mwegoha, kukamilika kwa ujenzi huo kutawezesha Kampasi kuanza kutekeleza majukumu yake na kutoa huduma mbalimbali zilizokusudiwa kwa jamii na wadau wengine.

Akizungumzia fursa zinazotokana na uwekezaji huo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, amesema uwepo wa Kampasi hiyo Mkinga ni fursa mpya ya maendeleo kwa jamii.

Amesema Kampasi hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji, huku mwingiliano kati ya wanafunzi, wataalamu na jamii ukiwa na nafasi muhimu katika kuchochea maendeleo ya eneo hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na wadau wengine kuhakikisha changamoto zinazoweza kuchelewesha matumizi ya Kampasi hiyo zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Aidha, Mhe. Kalima ametambua na kupongeza mchango wa viongozi wa vijiji waliowezesha upatikanaji wa eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 300 kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi hiyo.

Amesema upatikanaji wa eneo hilo umeweka msingi muhimu wa utekelezaji wa uwekezaji huo mkubwa, ambao unatarajiwa kuwa na manufaa ya muda mrefu kwa wananchi wa Mkinga na maeneo jirani.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...