Na. Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linaaendelea kujiimarisha katika Mafunzo na kutoa huduma Bora kwa Wananchi limeendelea kutoa mafunzo ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kuwajengea uwezo askari katika kutekeleza majukum kwa weledi na usasa ili kufanikisha adhima ya kutoa huduma bora kwa wananchi wanaolitegemea Jeshi hilo kwa ulinzi wao na mali.
Akiwaaga kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camillus Wambura Mkuu wa chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Dkt Lazaro Mambosasa amewataka Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wanaokwenda kuhudhuria mafunzo nchini Indonesia, kutumia vyema fursa hiyo kwa kuzingatia masomo watakayopatiwa na kuhakikisha maarifa na ujuzi watakaoupata unakuwa chachu ya kuleta tija, ufanisi na usasa katika utendaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, hususani katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi amesisitiza washiriki hao wanatakiwa kuzingatia nidhamu, weledi na maadili ya Jeshi la Polisi wakati wote watakapokuwa nchini Indonesia huku akiwataka kuwakilisha vyema Tanzania na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha wanakuwa na mwenendo unaotoa taswira nzuri ya nchi yetu.
Aidha amewataka washiriki hao kutumia fursa hiyo kuitangaza Tanzania kwa kuonyesha sifa njema ya nchi yetu katika kudumisha amani, usalama na utulivu, pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ambapo pia amewataka kutangaza maeneo ya kipekee yenye umuhimu wa kihistoria na kiutalii, ikiwemo Bonde la Ngorongoro, ambalo ni miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia.
Dkt Mambosasa amebainisha kuwa Mafunzo hayo yanatarajiwa kujikita katika maeneo mbalimbali muhimu, yakiwemo, Uongozi na Maendeleo ya Kitaaluma (Professional Development and Leadership), Ushirikishwaji wa Jamii katika Ulinzi na Usalama (Community Policing) Teknolojia Zinazochipukia (Emerging Technologies), ikiwemo Akili Bandia (AI) Matukio Makubwa na Mbinu za Uchunguzi wa Jinai (High-Profile Incidents and Criminal Investigative Techniques) Mbinu Bora za Utendaji na Ubunifu (Best Practices and Innovations).
Sambamba na hayo ameweka wazi kuwa Masomo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko na maboresho katika utendaji wa kazi za kila siku wa Jeshi la Polisi Tanzania, kwa kuwawezesha washiriki kupata maarifa, ujuzi na uzoefu mpya utakaosaidia kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukum ya Jeshi la Polisi.
Mafunzo hayo ya shirikisho la askari wa kike duniani na wasimamizi wa sheria IAWP yatahusisha nchi washiriki zaidi ya 64.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...