Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KAMPUNI ya Jubilee Life Insurance Tanzania imezindua bidhaa tatu mpya za bima ya maisha zinazolenga kuwasaidia Watanzania katika uwekaji akiba, maandalizi ya elimu, ulinzi wa maisha na mahitaji mengine ya kifedha ya baadaye.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bima hizo jijini Dar es Salaam Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Life Insurance Tanzania, Helena Mzena, amezitaja bima walizozindua ni Fanaka Plus, Smart Education Insurance Plan na Akiba Flex.

“Kwa miaka zaidi ya 10 tumekua tukitoa suluhisho la bima za maisha ambazo kimsingi zinampa mteja wetu nafasi ya kutimiza malengo yake aliyojiwekea kama vile kusomesha Watoto Pamoja na kukuza biashara zao huku wakiwa na ulinzi wa maisha yao.

“Kwa kujali na kuzingatia matakwa ya Watanzania wote, kwa Pamoja kama taasisi tumeona ni vyema kuendelea kuboresha bidhaa zetu hizi ili kuwa na manufaa zaidi kwa wateja wetu,”amesema Mzena 

Akieleza zaidi amesema bima yao kwa ajili ya uwekezaji ambayo ilikua ikijulikana kama FANAKA LIFE PLAN, sasa inaitwa FANAKA PLUS ikiwa na maboresho zaidi yanayomhakikishia mteja wetu ongezeko la fedha zake, ulinzi wa maisha yake Pamoja na amani ya moyo akijua hakuna janga au changamoto itayozuia utimiaji wa ndoto zake, yote haya na mengine mengi sasa yanapatikana ndani ya FANAKA PLUS.

Pia amesema wameboresha bima yetu ya Maisha ya Akiba flex ambayo yenyewe inamruhusu mteja wao kuchangia kwa ajili ya mkataba wake wa bima ya maisha huku ikimpa uhuru wa machangio yake pale anapohitaji.

“Hatukuwaacha nyuma wazazi ambao wanajali elimu ya Watoto wao, na rasmi tunatambulisha kwenu SMART EDUCATION, hii ni bima ya maisha kwa ajili ya maandalizi ya ada ya mtoto, hapa mteja wetu anaweka akiba yake ili kuhakikisha ndoto za kielimu za Watoto wake zinatimia…

“Huku akiwa na ulinzi wa maisha yake na uhakika wa kwamba sisi Jubilee Life Insurance tutawajibika kutimiza ndoto hizo hata bila uwepo wa huyu mzazi,”amesema.

Ameongeza bima zote hizo ni uthibitisho wa kwamba sisi kama taasisi tunajali na kuthamini ndoto za wateja wetu na kuhakikisha ndoto hizo zinafikiwa bila stress zozote.”Sisi tunasema, Bima ya Maisha ni ya kila mmoja.”

Kwa upande wake mwakilishi wa Kamishna kutoka TIRA, Alex Rocky amesema ubora wa bidhaa za bima haupaswi kupimwa kwa idadi ya watu waliojiunga pekee, bali pia kwa kiwango ambacho bidhaa hizo zinawawezesha wananchi kuelewa na kutumia huduma za bima kwa ufanisi.

“Uelewa hujenga imani, na imani huongeza matumizi endelevu ya bima,” amesema.

Amesema Tanzania inaingia katika hatua muhimu ya kujenga familia zenye uwezo wa kustahimili misukosuko ya kifedha na taifa lenye uimara wa kifedha, huku bima ya maisha ikiwa na nafasi muhimu katika kulinda wananchi na kusaidia mipango yao ya muda mrefu.

Amesema matumizi ya lugha ya Kiswahili katika bidhaa hizo ni hatua muhimu katika kuongeza uelewa na ujumuishi wa huduma za bima nchini.

“Matumizi ya lugha inayoeleweka katika kutoa taarifa na elimu kuhusu bima huwawezesha wananchi kuelewa kwa usahihi faida, masharti na wajibu wao kabla na baada ya kujiunga na bima,” amesema.

Pia amesema bima ya maisha ni nyenzo muhimu katika kujenga usalama wa kifedha na uwezo wa kustahimili changamoto kwa mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...