Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeandaa mwongozo utakaowawezesha wachungaji kuwafundisha waumini kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha, pamoja na kuwahimiza kuwa watulivu na kufuata taarifa na maelekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Serikali.
Akizungumza Septemba 16, 2026, jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Sita wa Wachungaji wa KKKT uliofanyika kwa siku tano, Mkuu wa KKKT, Askofu Alex G. Malasusa, amesema Kanisa limechukulia kwa uzito angalizo la TMA kuhusu mwenendo wa mvua za Oktoba hadi Disemba na limeanza kuchukua hatua za kuhakikisha taarifa hiyo inawafikia waumini kupitia wachungaji wao.
Amesema mwongozo huo utawasaidia wachungaji wanaporejea katika makanisa yao kuwafundisha waumini kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa, huku wakisisitiza umuhimu wa kufuata taarifa za kitaalamu na maelekezo ya Serikali kuhusu mwenendo wa mvua.
Askofu Malasusa amesema Kanisa lilianza maandalizi mara baada ya TMA kutoa angalizo hilo, likitumia ofisi zake kupanga namna bora ya kuwafikishia waumini ujumbe huo, huku Mkutano wa Wachungaji ukiwa fursa ya kuwapa viongozi hao taarifa na mikakati ya utekelezaji.
Ameeleza kuwa TMA ilitoa taarifa kwa umma Agosti 8, 2026, kuhusu mvua zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, ambapo baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua zilizo juu ya wastani au wastani, hususan Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini, Kanda ya Ziwa Victoria na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Amesema baadhi ya athari zinazoweza kujitokeza ni mafuriko, ongezeko la kina cha maji, magonjwa ya milipuko na changamoto katika uzalishaji wa baadhi ya mazao, huku sekta za utalii, ujenzi na usafiri zikitarajiwa kukumbwa na changamoto, ikiwemo mmomonyoko wa udongo.
Aidha, Askofu Malasusa amewataka waumini kuchukua tahadhari na kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka husika, akitolea mfano wa mafuriko yaliyotokea nchini Nepal na kusababisha vifo, huku akisema KKKT linawaombea wananchi wa nchi hiyo waliokumbwa na janga hilo.
Amesema waumini wanapaswa kuendelea kufanya maombi bila kuchoka, huku wakichukua hatua zinazohitajika, akitumia mfano wa watu wa wakati wa Nuhu ambao walipewa taarifa lakini hawakuzingatia, na baadaye wakakumbwa na madhara.
Katika hatua hiyo, amewataka waumini wa KKKT kufanya maombi maalumu katika ibada za Jumapili tatu mfululizo kuanzia Septemba 20, 2026, ambapo Jumapili ya kwanza wataombea familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na mafuriko nchini Nepal pamoja na kuiombea Serikali ya nchi hiyo ipate rasilimali za kuwahudumia wananchi walioathirika.
Amesema Septemba 27, 2026, maombi yataelekezwa kuiombea Tanzania ili Mungu aepushe janga la El Nino, pamoja na kuiombea Serikali ipate hekima, maarifa na rasilimali za kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Ameongeza kuwa Oktoba 4, 2026, yatafanyika maombi ya pamoja ya kumshukuru Mungu kwa imani, kwa kusikia maombi yaliyofanyika katika Jumapili hizo tatu mfululizo, amewataka waumini kuwa na imani na kuendelea kuchukua tahadhari, akisisitiza kuwa Mungu yupo na atawapitisha katika kila hali.


.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...