SERIKALI imesema inaendelea kuchukua hatua kuboresha kada ya madereva wa Serikali kwa kupanua fursa za ajira na kupanda madaraja, kuongeza mafunzo ya magari ya kisasa pamoja na kushughulikia changamoto za utoaji na uhuishaji wa leseni za udereva.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati akifungua Kongamano la Tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), lenye kaulimbiu “Dereva wa Serikali, Nguvu Moja, Sauti Moja, Kulinda Amani ya Nchi ni Jukumu Langu.”
Kasekenya amesema Serikali inatambua umuhimu wa kada hiyo kutokana na mchango wa madereva katika kuwawezesha viongozi, maafisa wa Serikali na watendaji mbalimbali kutekeleza majukumu yao, hivyo kuchangia katika utekelezaji wa shughuli za Serikali na ukuaji wa uchumi.
Akizungumzia maslahi na maendeleo ya kada hiyo, Kasekenya amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho ya miundo ya utumishi kwa lengo la kuongeza fursa za kupanda madaraja, maslahi na motisha kwa madereva wa Serikali.
Amesema amepokea ombi la kuhuishwa kwa mfumo wa madereva wa mitambo, yaani operators, pamoja na kupanuliwa kwa wigo wa upandishaji madaraja kwa madereva wa Serikali.
“Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kuratibu utekelezaji wa maboresho hayo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kasekenya amesema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa madereva wanawake wenye sifa, ili kuongeza idadi yao katika utumishi wa umma na kuimarisha usawa wa kijinsia katika kada hiyo.
Amesema madereva wanawake waliopo wameendelea kuonyesha utendaji mzuri, hivyo taasisi zinapaswa kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika ajira na utekelezaji wa majukumu.
Kasekenya amezitaka taasisi za umma ambazo hazina maafisa usafirishaji kuhakikisha zinakuwa na watumishi hao na kuwapa mafunzo yanayohitajika ili waweze kusimamia shughuli za usafirishaji na magari ya Serikali kwa ufanisi.
Aidha, amesema Serikali imetambua umuhimu wa kuwapatia madereva mafunzo ya matumizi ya magari ya kisasa yenye teknolojia mpya, kutokana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya usafiri.
Amesema Wizara ya Ujenzi itaendelea kuishauri Serikali ili taasisi za umma zitenge bajeti kwa ajili ya mafunzo ya mara kwa mara kwa madereva, hususan zinaponunua magari yenye teknolojia mpya.
Kuhusu changamoto ya utoaji na uhuishaji wa leseni za udereva, Kasekenya amesema Serikali inatambua kuwa leseni ni nyaraka muhimu inayomwezesha dereva kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Amesema mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha huduma za utoaji na uhuishaji wa leseni zinapatikana kwa wakati na kufanya tathmini ya taratibu zilizopo ili kuondoa vikwazo vinavyosababisha ucheleweshaji.
Pia amelitaka Jeshi la Polisi kutoa taarifa mapema kwa taasisi husika kuhusu mabadiliko ya leseni ili taasisi hizo ziweze kupanga na kutenga bajeti kwa ajili ya mahitaji hayo.
Wakati huo huo, Kasekenya amewataka madereva kuongeza umakini katika utekelezaji wa majukumu yao, kuzingatia sheria za usalama barabarani, kujiepusha na matumizi ya vilevi wakati wa kazi na kutumia kwa uangalifu magari ya Serikali wanayokabidhiwa.
Amesema matumizi ya teknolojia katika usalama barabarani, ikiwemo kamera za kufuatilia makosa ya barabarani, yanaendelea kuimarika, hivyo madereva wanapaswa kuzingatia sheria wakati wote wanapokuwa barabarani.
Kongamano hilo la Tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania limewakutanisha madereva kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujadili changamoto za kada hiyo na kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji wao katika utumishi wa umma.




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...