Na Farida Saidi Mangube, Morogoro
WAKATI wengine walipoona mwisho wa safari, Eva John aliona mwanzo wa maisha mapya.
Mwaka 2015, baada ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kiwangwa, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Eva alitamani kuendelea na masomo, lakini changamoto za maisha zilimlazimisha kusitisha safari yake ya elimu.
Badala ya kufungua ukurasa mpya wa masomo, maisha yake yaliingia katika kipindi kigumu kilichoambatana na shinikizo la kuolewa akiwa katika umri mdogo.
Akiwa bado na ndoto za kujijenga, Eva alilazimishwa kuingia katika ndoa mara tatu na wanaume tofauti. Baadhi yao walikuwa tayari na wake wengine, huku wengine wakimtaka awe mke wa nyumbani asiyehusika katika shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, Eva hakukubali hali hiyo iwe hatima ya maisha yake.
Mwaka 2017, aliamua kuanza kujenga maisha yake kwa kujikita katika shughuli za kilimo. Alianza kwa kuomba ardhi kwa ndugu zake na kutafuta namna ya kujipatia kipato kupitia kilimo ili aweze kujikimu.
Mwaka 2018 alianza rasmi kujitegemea baada ya kununua shamba lenye ukubwa wa ekari moja, hatua iliyokuwa mwanzo wa safari iliyombadilisha kutoka mwanamke aliyekuwa akitegemea maamuzi ya wengine hadi kuwa mkulima, mjasiriamali na mwajiri.
Tatizo la mazao likawa fursa
Mwaka 2018, Eva alianza kilimo cha nanasi akiwa na ekari moja.
Kama ilivyo kwa wakulima wengi wanaotegemea kilimo kama chanzo cha kipato, changamoto hazikuwa chache. Uzalishaji ulikuwa mdogo, ujuzi ulikuwa bado unaendelea kujengwa na masoko hayakuwa ya uhakika.
Wakati mwingine mazao yalibaki shambani na kuharibika kutokana na kukosa wanunuzi.
Badala ya kukiona kilimo kama shughuli ya kuzalisha na kuuza mazao ghafi pekee, Eva alianza kutafuta namna ya kuongeza thamani ya mazao na kupunguza upotevu baada ya mavuno.
Hapo ndipo safari yake kutoka mkulima mdogo hadi mjasiriamali wa kilimo ilipoanza kuchukua mwelekeo mpya.
Leo, shughuli zake kupitia MJASI Enterprises zinahusisha uzalishaji na usindikaji wa mazao mbalimbali, yakiwemo mananasi, nyanya na mbogamboga.
Sh milioni 44.5 zafungua ukurasa mpya
Mabadiliko makubwa katika biashara yake yalikuja baada ya kupata mkopo wa Sh milioni 44.5 usio na riba kutoka shirika la CAMFED, kupitia mpango wa kuwawezesha wasichana na wanawake wanachama wa CAMA kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.
Kwa Eva, fedha hizo hazikuwa tu mtaji wa biashara, bali zilikuwa fursa ya kubadili ukubwa na mwelekeo wa shughuli zake.
Alizielekeza katika kuongeza uwezo wa uzalishaji, ikiwemo kununua mashine za kukausha mazao na kupanua shughuli zake za kilimo.
Mashine hizo zimemwezesha kwenda hatua zaidi ya kuuza mazao ghafi kwa kuyaongezea thamani na kuyafanya yaweze kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi.
Uwekezaji huo pia umemsaidia kupanua wigo wa uzalishaji.
Kutoka kutegemea zaidi mananasi, sasa ameanza kulima dragon fruit, huku akilenga kuongeza aina ya mazao, fursa za biashara na uzalishaji shambani.
Kwa sasa, anamiliki takribani ekari 10, kutoka ekari moja aliyokuwa nayo mwaka 2018.
Shamba lililogeuka kuwa chanzo cha ajira
Mafanikio ya Eva hayaishii katika ukubwa wa shamba.
Kupitia MJASI Enterprises, ameajiri wafanyakazi wanne, wakiwemo mwanamke mmoja na wanaume watatu, wanaomsaidia katika shughuli mbalimbali za shamba.
Aidha, zaidi ya watu 10 hupata ajira zisizo rasmi kulingana na msimu, hususan katika shughuli za kilimo na uzalishaji.
Hivyo, kile kilichoanza kama juhudi ya mwanamke mmoja kutafuta maisha, sasa kimeanza kuwa chanzo cha kipato kwa watu wengine.
Hapo ndipo maana pana ya uwezeshaji wa kiuchumi inapojitokeza, kwani mwananchi anapopata fursa ya kukuza shughuli yake, matokeo yanaweza kuvuka mipaka ya kaya yake na kuwafikia watu wengine katika jamii.
Kutoka kukatisha masomo hadi kusaidia watoto wengine
Pengine sehemu inayogusa zaidi katika simulizi ya Eva si ukubwa wa shamba lake wala thamani ya mkopo alioupata, bali kile anachofanya baada ya kufikia mafanikio hayo.
Kwa sasa, Eva anawasaidia wanafunzi 13 katika eneo analoishi kwa kuwapatia mahitaji ya shule ili waendelee na masomo.
Yeye mwenyewe alifikia kidato cha nne lakini hakupata nafasi ya kuendelea na elimu kutokana na changamoto za maisha.
Changamoto hiyo, ambayo wakati mmoja ilikuwa chanzo cha maumivu na dharau kutoka kwa baadhi ya watu, sasa imekuwa msukumo wa kuwasaidia watoto wengine wasikatize safari yao ya elimu.
Safari ya Eva inaingia katika mjadala mpana wa kitaifa kuhusu namna ya kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kujenga uwezo wa kiuchumi.
NEEC: Uwezeshaji si kutoa fedha pekee
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bengil Issa, anasema uwezeshaji wa wananchi haupaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa kutoa fedha pekee.
Kwa mujibu wa Bengil, Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unahitaji wananchi kuunganishwa na fursa zinazowawezesha kuzalisha, kukuza biashara na kuongeza kipato.
“Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi unahitaji kuangalia mnyororo mzima wa thamani. Mwananchi anapopata mtaji, anahitaji pia kuwa na ujuzi, teknolojia, taarifa, masoko na huduma zinazomwezesha kutumia fursa hiyo kwa tija,” anasema.
Anaeleza kuwa kilimo ni miongoni mwa maeneo yenye nafasi kubwa ya kuzalisha ajira na kipato pale kinapounganishwa na usindikaji, teknolojia na masoko.
“Tunataka kuona wananchi wakitoka kwenye uzalishaji wa kawaida kwenda kwenye shughuli zinazoongeza thamani. Hii inasaidia kuongeza kipato cha mzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao na pia kufungua fursa nyingine katika mnyororo wa thamani,” anasema.
CAMFED na daraja kutoka elimu hadi kujitegemea
Kwa upande wa CAMFED, safari ya Eva ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wasichana na wanawake kupitia elimu, ujuzi na fursa za kiuchumi.
Akizungumza katika maadhimisho ya mafanikio ya mwaka 2025 ya mtandao wa CAMA, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED, Anna Sawaki, alisema ushirikiano kati ya CAMFED, Serikali na wadau mbalimbali umesaidia kuwaandaa wasichana kupata elimu, ujuzi wa ufundi, mikopo na fursa za kujitegemea.
“Lengo letu ni kumfanya mtoto wa kike aweze kujitegemea yeye mwenyewe, kuisaidia familia yake na hatimaye kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa ujumla,” alisema Sawaki.
Kwa mujibu wa CAMFED, zaidi ya wasichana 100,000 kutoka mikoa 10 ya Tanzania wamefikiwa kupitia mipango ya elimu na uwezeshaji, huku zaidi ya wasichana 34,000 wakinufaika mwaka 2025 pekee.
Mwenyekiti wa mtandao huo, Shamsa Mkuruno, amesema wanachama 511 wamepata mikopo isiyo na riba kutoka CAMFED, huku wengine wakijikita katika kilimo, ushonaji, useremala, ufundi wa chuma na shughuli za kuongeza thamani ya bidhaa na mazao.
Mafanikio yanayovuka mipaka ya kaya
Kisa cha Eva kinaonyesha kwamba thamani ya uwezeshaji haiishii katika kiasi cha fedha anachopokea mwananchi.
Thamani yake inaonekana katika kile kinachotokea baada ya fursa hiyo kupatikana.
Kwa Eva, Sh milioni 44.5 zimegeuka kuwa mashine za usindikaji, uzalishaji mkubwa, upanuzi wa mashamba, zao jipya, ajira na vyanzo vipya vya mapato.
Kwa familia yake, mafanikio hayo yameambatana na kujenga nyumba, kuwasaidia wazazi na kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji ya kila siku.
Kwa jamii, yamezalisha ajira na shughuli za kiuchumi.
Na kwa watoto 13 anaowasaidia, mafanikio hayo yamekuwa sehemu ya jitihada za kuhakikisha changamoto za kiuchumi hazikatizi ndoto zao za elimu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED Anna Sawaki Akizungumza na wanahabari katika maadhimisho ya mafanikio ya mwaka 2025 ya mtandao wa CAMA yaliyofanyika Mjini Morogoro


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...