Na Janeth Raphael - MichuziTv Bungeni Dodoma 

Mafunzo kwa vijana yanatarajiwa kwenda zaidi ya kuwapatia ujuzi, huku msisitizo ukiwekwa katika kuwaunganisha na ajira, mitaji, masoko na fursa za uzalishaji ili waweze kujiajiri na kuanzisha biashara endelevu.

Hayo yameelezwa Bungeni na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Zulfa Mmaka Omary, aliyetaka kujua namna Serikali inavyohakikisha programu za mafunzo na uwezeshaji kwa vijana zinazalisha ajira halisi na endelevu.

Zulfa alihoji kuhusu mkakati mahsusi wa kuhakikisha ajira na uwezeshaji wa vijana haviishii katika kuwapatia mafunzo pekee, bali vinawasaidia vijana kupata ajira, kujiajiri na kuwa na shughuli za kiuchumi zenye uwezo wa kudumu.

Akijibu, Naibu Waziri Katimba amesema mafunzo yanayotolewa kwa vijana yanaelekezwa zaidi katika mahitaji ya soko la ajira na fursa zilizopo katika shughuli za uzalishaji.

Amesema hatua hiyo inaambatana na mafunzo kwa vitendo, uanagenzi na kuwapatia vijana uzoefu wa kazi, sambamba na kuwaunganisha na mitaji, vifaa na zana za uzalishaji.

 Katimba, amesema mkakati huo unatekelezwa kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji vijana, zikiwemo Programu ya Kukuza Ujuzi, Build for Better Tomorrow, Mining for a Brighter Tomorrow, pamoja na Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi yenye Shilingi bilioni 200.

Programu nyingine ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, pamoja na programu zinazotekelezwa na SIDO na VETA.

Aidha, amesema vijana wanaunganishwa na waajiri, taasisi za fedha, wawekezaji, masoko pamoja na fursa za ununuzi wa umma ili kuwawezesha kutumia ujuzi walioupata katika kupata ajira au kuanzisha na kukuza biashara zao.

Amesema uwezeshaji huo unaenda sambamba na ushauri wa kitaalamu, uatamiaji wa biashara, uunganishaji wa vijana katika minyororo ya thamani na masoko, pamoja na ufuatiliaji wa miradi wanayoianzisha.

Hatua hizo, kwa mujibu wa Naibu Waziri, zinalenga kuhakikisha vijana wanapata mazingira yanayowawezesha kutumia ujuzi wao kuzalisha kipato, kujenga biashara zinazodumu na hatimaye kutoa ajira kwa vijana wengine.

Amesema utekelezaji wa mikakati hiyo unafanyika kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau wengine wa maendeleo, kwa lengo la kujenga mfumo unaomsaidia kijana kuanzia hatua ya kupata mafunzo hadi kufikia ajira, kujiajiri au kukuza biashara yenye tija.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...