Na Janeth Raphael - MichuziTv Bungeni Dodoma


SERIKALI imesema itaendelea kuboresha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kuimarisha matumizi ya wataalamu wa mafunzo ya biashara, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na manufaa ya mikopo hiyo kwa wajasiriamali nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Dkt. Festo Dungange, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Athman Issa.

Katika swali lake, Mbunge Chiku alitaka kujua iwapo Serikali inaona kuwa sababu kubwa ya mikopo ya asilimia 10 kutokuwa na matokeo makubwa tangu kuanza kwake ni ukosefu wa wataalamu wa kutoa mafunzo ya biashara kwa wanufaika.

Akijibu, Dkt. Dungange amesema Serikali inaendelea kutoa mikopo hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, pamoja na Kanuni zake za mwaka 2024, ambazo zinaweka utaratibu wa ukopaji, urejeshaji na usimamizi wa mikopo hiyo.

Amesema lengo la mikopo hiyo ni kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mitaji midogo na ya kati isiyo na riba kupitia mapato ya ndani ya halmashauri, ili kuwawezesha kuendesha shughuli za ujasiriamali na kurejesha mikopo kwa ajili ya kuwanufaisha wajasiriamali wengine.

Dkt. Dungange amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 hadi 2025/26, jumla ya vikundi 33,594 vya wajasiriamali vilinufaika na mikopo hiyo.

Amefafanua kuwa kati ya vikundi hivyo, 18,539 vilikuwa vya wanawake, 11,758 vya vijana na 3,247 vya watu wenye ulemavu, huku jumla ya Sh bilioni 357.20 zikitolewa kwa vikundi hivyo.

Dkt. Dungange, amesema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 143.43 zilikuwa zimefikia muda wa marejesho, ambapo Sh bilioni 130.04, sawa na asilimia 91, zilikuwa tayari zimerejeshwa.

Aidha, amesema Serikali tayari imeweka mwongozo unaowataka wataalamu wa fedha, maendeleo ya jamii na wataalamu wengine waliopo katika halmashauri kushiriki katika kuwaelimisha na kuwasimamia wajasiriamali wanaoomba mikopo hiyo.

Amesema mwongozo huo pia umeweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya masuala ya fedha na ujasiriamali kwa vikundi vinavyoomba mikopo, hatua inayolenga kuwajengea uwezo wa kutumia vizuri fedha wanazokopa na kuongeza uwezekano wa mafanikio katika shughuli zao.

“Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wajasiriamali kwa kuwatumia wataalamu wa mafunzo ya biashara ili kuongeza ufanisi wa mikopo hiyo,” alisema Dkt. Dungange.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...