Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amefanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Mto Ng’ombe, Tandale jijini Dar es Salaam, kukagua hali ya usafi wa mazingira na maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika kipindi cha mvua.

Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Waziri wa TAMISEMI pamoja na viongozi wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Ndejembi ameelekeza Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha mto huo unasafishwa na taka zilizorundikana kandokando ya Mto Ng’ombe zinaondolewa haraka na mazingira yanaendelea kuwekwa katika hali ya usafi.

Amewaagiza Viongozi wa Halmshauri, kupitia maafisa mazingira na maafisa maendeleo, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuzingatia usafi na ukusanyaji wa taka. Amesema ni muhimu kwa Halmashauri kuweka miundombinu mizuri ya kukusanya taka na kuzichukua kwa wakati ili wananchi wasitupe taka hizo katika maeneo yasiyofaa.

Vilevile, ameelekeza mamlaka za Wilaya ya Kinondoni kuweka utaratibu wa maeneo rasmi ya kutupa taka ili wananchi wawe na sehemu zinazotambulika kwa ajili ya kuhifadhi taka, hatua itakayosaidia kudhibiti utupaji holela na uchafuzi wa mazingira.

Akizungumza na wananchi wanaoishi pembezoni mwa Mto Ng’ombe, Makamu wa Rais amewataka kuzingatia usafi wa mazingira na kubadili tabia ya utupaji taka holela, akisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unahitaji ushiriki wa Serikali na wananchi kwa pamoja.

Aidha, Makamu wa Rais ameelekeza madaraja yanayokatiza maeneo ya Pakacha na Sokoni katika Mto Kiboko yanapitika wakati wa mvua, ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila kukwamishwa na changamoto za miundombinu.

















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...