Na Said Mwishehe,Michuzi TV HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imesema viongozi wakuu wa kitaifa wameweka msisitizo wa kuhakikisha Jiji hilo linakuwa safi wakati wote, hivyo Jiji hilo limewahimiza wananchi kuwa sehemu ya juhudi hizo kuhakikisha mazingira yanakuwa safi.

Akizungumza leo Septemba 5,2026 wakati akishiriki usafi katika soko la Buguruni, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya amesema pia ushiriki wa wananchi katika zoezi la usafi umeendelea kuimarika, huku viongozi kutoka ngazi mbalimbali nao wakishiriki katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Amesema usafi wa mazingira jijini humo hufanyika kwa ushirikiano wa viongozi na wananchi, ambapo zoezi la usafi hufanyika kila Jumamosi pamoja na kuendelea kuhamasisha usafi katika siku nyingine za wiki.

Mkurugenzi huyo amesema utekelezaji huo unaendana na maelekezo, sera na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha kila mmoja anakuwa sehemu ya usafi na kujenga utamaduni wa kushirikiana katika kulinda mazingira.

Amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaendelea kusimamia Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Sera ya Taifa ya Mazingira kwa kuhakikisha mipango ya usafi na utunzaji wa mazingira inatekelezwa ipasavyo.

Katika hatua nyingine, amesema Jiji linaelekea katika mwelekeo mpya wa usimamizi wa taka, ikiwemo ukusanyaji, usafirishaji na utupaji wa taka, huku sekta binafsi ikitarajiwa kushirikishwa zaidi kuongeza nguvu katika juhudi za kulifanya Dar es Salaam kuwa safi.

Ametoa wito kwa wananchi katika kata zote za Jiji hilo pamoja na viongozi ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha mazingira ya jiji yanakuwa safi wakati wote.

Amesema maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika suala la usafi ni pamoja na mitaro, barabara, masoko, miundombinu ya umma na maeneo ya makazi ya wananchi.

Kuhusu wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi, Mkurugenzi huyo amesema Halmashauri inaendelea kutekeleza utaratibu maalumu wa kuhakikisha wafanyabiashara hao wanahamishiwa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya biashara.

Amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakipanga biashara zao kandokando ya barabara na kusababisha msongamano, hali ambayo amesema si salama na haiendani na mipango ya matumizi bora ya maeneo ya jiji.

Amesema katika zoezi lililofanyika eneo la Soko la Buguruni, baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wamepanga biashara zao nje ya soko wameelekezwa na kurejea ndani ya soko baada ya kutambua kuwa eneo walilokuwa wakifanyia biashara halikuwa sahihi.

Mkurugenzi huyo amesema mpango wa kuwapanga wafanyabiashara unaendelea, huku Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikitenga Shilingi bilioni 6.7 katika mwaka wa fedha kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na uzalishaji wa masoko.

Amesema lengo la mpango huo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi wanapata maeneo sahihi ya kufanyia biashara kupitia masoko yanayojengwa na kukarabatiwa na Halmashauri.

Aidha, amesema kwa ridhaa na baraka za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mpango wa ujenzi wa soko la kisasa eneo la Jangwani, maarufu kama Figo Sambusa, unaendelea kwa ajili ya kuwahudumia machinga na wafanyabiashara wadogo.

Amesema soko hilo linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 80, hatua ambayo amesema inaonyesha dhamira ya Serikali ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kupata maeneo rasmi ya biashara, kujikwamua kiuchumi na kuwa sehemu muhimu ya kuchangia katika pato la Taifa.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...