ZANZIBAR
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Ndugu Abdi Mahamoud Abdi, amepongeza hatua za utekelezaji wa mradi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, akisema kukamilika kwake kutachochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Abdi ameyasema hayo leo, Septemba 20, 2026, wakati akiendelea na ziara yake katika Jimbo la Bumbwini, ambapo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar inayojengwa Mangapwani.
Amesema CCM imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa katika utekelezaji wa mradi huo, ambao unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na biashara Zanzibar.
Aidha, amempongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendelea kutekeleza ahadi za Serikali kwa vitendo, ikiwemo ujenzi wa bandari hiyo ya kisasa.
Ndugu Abdi amesema ujenzi wa Bandari ya Mangapwani utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan katika maeneo ya Kaskazini Unguja, pamoja na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazozunguka bandari hiyo.
Amesema bandari hiyo pia itakuwa na nafasi muhimu katika uhifadhi wa mafuta, hatua ambayo itasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa bidhaa hiyo na kuimarisha upatikanaji wake wakati wa mabadiliko ya bei katika masoko mbalimbali.
“Ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ni miongoni mwa hatua zinazoonesha namna Zanzibar inavyoendelea kufunguka katika maendeleo endelevu kupitia sekta ya bahari na uchumi wa buluu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, amesema mradi huo unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 30 hadi kukamilika kwake.
Naye Mkandarasi wa Mradi wa Mafuta na Gesi Asilia Mangapwani, Salum Udi, amesema kutokana na kina cha maji katika eneo hilo, bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa zenye uwezo wa kubeba hadi makontena 20,000.
Amesema ujenzi wa bandari hiyo pia utahusisha miundombinu mbalimbali ya kisasa, ikiwemo bandari ya mafuta na gesi asilia, miundombinu ya kijamii, upatikanaji wa maji safi na salama, viwanja vya michezo pamoja na maeneo ya mapumziko kwa wananchi.



.jpeg)

.jpeg)



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...