Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeratibu na kuendesha semina mtandao (Webnar) maalum ikilenga kuwahamasisha Watanzania kutumia fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji na hisa nchini hususani kupitia maendeleo ya teknolojia yaliyorahisisha ufikiwaji wa masoko hayo hadi kupitia njia ya simu za mikononi.

Semina hiyo iliyorushwa moja kwa moja mtandaoni kutoka makao makuu ya benki hiyo iliwahusisha wadau tofauti waliowakilisha taasisi wasimamizi ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

Akizungumza katika semina hiyo, ambayo pamoja na mambo mengine ilijadili namna wananchi hususani wa kipato cha chini wanavyoweza kutumia akaunti zao za benki kufikia masoko ya mitaji, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema kwasasa ni wakati muafaka kwa watanzania kutumia taasisi za fedha kama vituo vya elimu kwenye masuala muhimu ya uwekezaji tofauti utamaduni uliojengeka wa taasisi hizo kutumika kama sehemu ya kuweka akiba na mikopo.

“Na hii ndio sababu kama benki tunawekeza zaidi kwenye mifumo inayowawezesha wateja wetu kushiriki katika uwekezaji wa masoko ya mitaji. Yaani kwamba sasa benki ni zaidi ya kuweka akiba na kukopa bali ni kuinganishi muhimu cha elimu na huduma za kuyafikia masoko ya mitaji na soko la hisa,” alisema Sabi.

Alitolea mfano wa huduma ya NBC Kiganjani ambayo imeunganishwa na DSE Kiganjani, huku mifumo ya mifuko ya uwekezaji ya UTT na iTrust nayo ikiwa imeunganishwa na huduma hiyo na huduma nyingine zikiwa katika hatua za kuunganishwa.

Alitoa wito kwa Watanzania wenye fedha kuacha kuzihifadhi bila kuzalisha thamani na badala yake kuzitumia katika fursa mbalimbali za uwekezaji, ikiwemo hisa na hati fungani za Serikali.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela, alisema safari ya uwekezaji katika masoko ya mitaji si ngumu kama inavyodhaniwa, kutokana na kurahisishwa kwa huduma kupitia simu za mkononi na upatikanaji wa ushauri wa uwekezaji kupitia matawi ya benki.

Alisema licha ya idadi ya wawekezaji kwenye masoko ya mitaji nchini kuongezeka na kufikia takribani 900,000, bado idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Watanzania inayokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 70.

“Naendelea kuwahimiza wananchi kutokuona uwekezaji kama shughuli inayohitaji kuwa na mamilioni ya fedha, na msisitizo wangu kwao ni kwamba mtu yeyote anaweza kuanza kwa kiasi kidogo, ikiwemo Sh5,000 au Sh20,000, kutegemea bidhaa na masharti ya uwekezaji husika.’’ Alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Alfred Mkombo, alisema mamlaka hiyo inaendelea kusimamia masoko ya mitaji kwa lengo la kulinda maslahi ya wawekezaji na kuhakikisha wanafanya maamuzi wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu uwekezaji wanaoufanya.

Mkombo aliwashauri wawekezaji kutoweka fedha zao zote katika eneo moja, bali kugawanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali kama hati fungani, mifuko ya uwekezaji wa pamoja, nyumba na makazi pamoja na amana za muda maalumu benki.

Naye Emmanuel Akaro, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alisema benki hiyo inaendelea kufanya maboresho yenye lengo la kuongeza wigo wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika masoko ya mitaji.

Alisema kuna fedha nyingi ambazo hazipo kwenye mzunguko wa uchumi na kwamba kuna umuhimu wa kuwa na mikakati ya kuwahamasisha wamiliki wa fedha hizo kuziwekeza katika maeneo kama hati fungani, benki na mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

“Tangu mwezi Julai, baada ya mabadiliko ya sheria yaliyofungua akaunti ya mitaji, wawekezaji kutoka nje wakiwemo Diaspora wamewezeshwa kushiriki katika soko la dhamana za Serikali hatua inayowawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi, ikiwemo wale ambao watoto wao hawana uraia wa Tanzania, kuwekeza katika hati fungani za Serikali na kunufaika na uwekezaji huo.’’ Alisema.

Akizungumzia semina mtandao (Webnar) hiyo, Sarah Laizer Sumaye, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Udhibiti (Director of Compliance and Regulatory Affairs) wa NBC, alisema ilikuwa sehemu ya mpango endelevu wa benki wa kutoa elimu kwa wateja kuhusu fursa mbalimbali za kifedha.

Alisema webinar hiyo, iliyowakutanisha wataalamu kutoka NBC, DSE, CMSA na BoT, imelenga hasa kumsaidia Mtanzania wa kawaida kuelewa namna anavyoweza kutumia huduma za benki kufikia masoko ya mitaji na kuwekeza kwa ajili ya malengo yake ya kifedha.

“Hatutaishia kwenye akiba na mikopo. Tunataka kuwapa wateja wetu fursa mbalimbali, ikiwemo fursa za uwekezaji endelevu,” alisema.

Sumaye alisema NBC itaendelea na programu hiyo ya elimu kupitia mpango wa Compliance Advocacy Program, ambapo pamoja na masoko ya mitaji, benki hiyo itaendelea kutoa elimu kuhusu maeneo mengine yakiwemo Mazingira, Jamii, na Utawala (ESG), Faragha ya Taarifa (Data Privacy) na Maadili ya Biashara (Business Ethics)
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum iliyoandaliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha. Semina hiyo imelenga kuhamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya mitaji na hisa nchini, hususan kupitia teknolojia ya simu za mkononi. Waliopo meza kuu kutoka kushoto: Ibrahim Nzutu, Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Biashara NBC (Muendesha Semina), Peter Nalitolela, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Theobald Sabi, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Emmanuel Akaro, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Alfred Mkombo, Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango (CMSA)




Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum iliyoandaliwa na benki ya NBC kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha. Semina hiyo imelenga kuhamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya mitaji na hisa nchini, hususan kupitia teknolojia ya simu za mkononi. Kulia meza kuu ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi na Ibrahim Nzutu, Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Biashara NBC (Muendesha Semina)


Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Alfred Mkombo, (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum iliyoandaliwa na benki ya NBC kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha. Semina hiyo imelenga kuhamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya mitaji na hisa nchini, hususan kupitia teknolojia ya simu za mkononi.


Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Akaro, (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza wakati wa semina mtandao (webinar) maalum iliyoandaliwa na benki ya NBC kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha. Semina hiyo imelenga kuhamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya mitaji na hisa nchini, hususan kupitia teknolojia ya simu za mkononi.


Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wakiwemo maofisa waandamizi wa benki ya NBC, CMSA, BOT na DSE wakifuatilia mijadala kutoka kwa wawasilishaji.


Akizungumzia semina mtandao (Webnar) hiyo, Sarah Laizer Sumaye (alieshika mic) ambaye Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Udhibiti (Director of Compliance and Regulatory Affairs) wa NBC, alisema ilikuwa sehemu ya mpango endelevu wa benki wa kutoa elimu kwa wateja kuhusu fursa mbalimbali za kifedha.


Semina hiyo iliyorushwa moja kwa moja mtandaoni kutoka makao makuu ya benki ya NBC iliwahusisha wadau tofauti waliowakilisha taasisi wasimamizi ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...