Nyerere Cycling Tour Imetangaza washirika wa safari ya mwaka huu itakayokuwa na umbali wa kilomita 1,500 hadi Butiama, huku Vodacom Tanzania ikiendelea kuwa mshirika mkuu wa msafara huo, ikishirikiana na Afro Oil, Stanbic Bank Tanzania, BYD, ABC Bicycle, Coca-Cola na Huawei.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Zuweina Farah, alisema Vodacom itaendelea kushirikiana na Nyerere Cycling Tour kama mshirika mkuu, akieleza kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya kampuni ya kuendelea kuunga mkono mipango yenye kuleta matokeo chanya kwa jamii nchini.
Alisema Vodacom pia inafurahia kuwapokea washirika wapya ambao ushiriki wao utaongeza thamani katika safari ya mwaka huu na kusaidia kupanua wigo na matokeo ya msafara huo.
Msafara huo utafanyika kuanzia tarehe 5 hadi 14 Oktoba 2026, ukiwa na mkazo katika elimu, afya na uhifadhi wa mazingira, sambamba na kuhamasisha wanafunzi, hususan wasichana, kushiriki katika michezo ya kuendesha baiskeli.
Katika safari ya mwaka huu, Vodacom wanatarajia kutoa madawati 1,000 kwa shule 10, kukarabati madarasa 40 na kujenga madarasa mapya 10, huku shughuli hizo zikitarajiwa kuwafikia zaidi ya wanafunzi 25,000. Katika safari zilizopita, Nyerere Cycling Tour ilifikia shule 107 na zaidi ya wanafunzi 75,000 walinufaika.
Akizungumzia ushirika wao, Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Mkini, alisema benki hiyo itatumia msafara huo kuhamasisha elimu ya fedha kwa wanafunzi na vijana, ili kuwajengea uelewa itakayowasaidia kufanya maamuzi bora kuhusu matumizi na usimamizi wa fedha.
Kwa upande wake, Afro Oil imesema ushiriki wake unatokana na dhamira ya kampuni ya kurudisha kwa jamii, huku Samwel Msonsa kutoka BYD alisema kampuni hiyo itashiriki katika uzalishaji na uhamasishaji wa msafara huo, pamoja na shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji miti.
Msafara huo hadi sasa umesajili waendesha baiskeli 213, huku wengine wakitarajiwa kujiunga njiani. Waendesha baiskeli kutoka nchi 12 wanatarajiwa kushiriki, zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Afrika Kusini, Australia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uholanzi. Aidha, wanawake 23 tayari wamesajiliwa kushiriki katika msafara huo.
Vodacom pia ilitoa taarifa kuhusu Vodacom Coastal Classic, ambayo hadi sasa imeandikisha washiriki 147. Na washindi wa nafasi ya kwanza kwa wanawake na wanaume watapata Sh milioni 10 kila mmoja, nafasi ya pili Sh milioni 7 na nafasi ya tatu Sh milioni 5. Waendesha baiskeli watakaomaliza nafasi ya nne hadi ya kumi watapata Sh milioni 1 kila mmoja.
Vodacom Tanzania imewekeza Sh milioni 160 katika Msafara wa Baiskeli wa Nyerere, huku Vodacom Foundation ikichangia zaidi ya Sh milioni 300 kwa shughuli za kijamii zitakazotekelezwa katika maeneo yatakayopitiwa na msafara huo, ikiwemo uboreshaji wa shule na utoaji wa madawati. Safari hiyo itahitimishwa Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Washirika wa Nyerere Cycling Tour, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania PLC, Zuweina Farah (wa nne kulia), ambaye aliwakilisha Vodacom Tanzania PLC kama mdhamini mkuu wa msafara huo, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano na waandishi wa habari na wadau wa msafara huo uliolenga kutangaza rasmi washirika wa zamani na wapya wa msafara huo. Katika picha kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Afroil, Mohamed Al-Jabry(wa pili kushoto) Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Nkini (wa tatu kushoto), Mkuu wa Masoko na Mauzo wa BYD, Samwel Msonsa (wanne kushoto), Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, Meneja wa Akaunti wa Vodacom Huawei, Victor Wang, na Katibu Mtendaji wa Coca-Cola Tanzania, Yvette Gadi. Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 2026
Baadhi ya washiriki wa msafara wa Nyerere cycling tour wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari na wadau wa msafara huo uliolenga kutangaza rasmi washirika wa zamani na wapya wa msafara huo.
Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour Gabriel Landa (wa kwanza kulia) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari na washirika wao. Majadiliano hayo yalihusu namna gani watajumuika katika msafara huo.

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...