MOSHI
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewaagiza wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao chini katika barabara zinazozunguka Soko la Mbuyuni, Manispaa ya Moshi, kuondoka katika maeneo hayo na kuhamia ndani ya soko hilo ili kuepuka milipuko ya magonjwa na uchafuzi wa mazingira.
Babu alitoa agizo hilo jana wakati akishiriki zoezi la usafi katika Soko la Mbuyuni, ambapo alisema barabara zimejengwa kwa ajili ya kupitisha magari na wananchi, hivyo hazipaswi kutumika kama maeneo ya kufanyia biashara.
Alisema wafanyabiashara wanaofanyia biashara pembezoni mwa barabara wanapaswa kufika kwa viongozi wa soko hilo ili kupangiwa maeneo rasmi ya kufanyia biashara, kabla Serikali haijachukua hatua za kuwaondoa katika maeneo hayo.
“Niwaombe muanze kuondoka wenyewe mapema, tusije tukaja kuwaondoa sisi mkasema tunawaonea. Serikali imetumia fedha nyingi kujenga masoko haya, hivyo ni wajibu wenu kufanya biashara ndani ya masoko haya ambayo yamewekewa miundombinu rafiki ya kuwahudumia,” alisema Babu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema wafanyabiashara hao wakijipanga na kufanya shughuli zao ndani ya soko, wateja wataendelea kuwafuata huko kwa ajili ya kununua bidhaa.
Alisisitiza kuwa agizo hilo linapaswa kutekelezwa bila shuruti, akiwataka wafanyabiashara kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa kwa ajili ya kuhakikisha usalama, usafi na ustawi wa wananchi.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...