Na. Jawadu Kinyobwa
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Chama Cha Wafanyakazi Madaktari na Wafamasia Tanzania katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wataalamu hao, huku ikisisitiza umuhimu wa maslahi ya watumishi kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Ndege Qwaray, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Pili wa Chama cha Wafanyakazi wa Madaktari na Wafamasia Tanzania, leo Septemba 18, 2026.
Amesema Serikali inatambua nafasi ya vyama vya wafanyakazi katika kujenga mahusiano bora kazini, kuwakilisha maslahi ya wanachama na kusaidia kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya kazi.
Amesema Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Afya, ambapo idadi ya vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka 10,153 mwaka 2021/22 hadi 13,683 Machi 2026, sawa na ongezeko la vituo 3,530.
Aidha, Serikali imejenga hospitali mpya 10 za rufaa za mikoa, kukarabati hospitali kongwe 50, kukamilisha maboma 980 ya zahanati na kujenga vituo vipya vya afya 390, sambamba na kuongeza vifaa tiba vya kisasa ikiwemo CT Scan na MRI.
Katika eneo la rasilimali watu, Mhe. Qwaray amesema Serikali imeajiri zaidi ya watumishi wa afya 53,633 wa kada mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025/26.
Mhe. Qwaray amesisitiza kuwa Serikali inatambua mchango wa Madaktari na Wafamasia katika kujenga Taifa lenye afya bora na itaendelea kushirikiana na chama hicho pamoja na wadau wengine wa Sekta ya Afya katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo.
Amesema katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni muhimu waendelee kujenga utaalamu, kufanya tafiti, kubuni njia mpya za utoaji huduma na kutumia teknolojia kuboresha afya za wananchi.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...