Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kuchukua hatua za kuboresha ustawi wa punda nchini, ikiwemo kuingiza masuala ya mnyama huyo katika mitaala ya mafunzo ya wataalamu wa mifugo kuanzia ngazi ya cheti na diploma pamoja na kuandaa mwongozo maalumu wa matibabu ya punda.

Hayo yamebainishwa Septemba 23, 2026, katika kikao Maalum kati ya wadau wa Mnyama punda na Ofisi ya Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, ambapo Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania, Dkt. Benezeth Lutege Malinda, amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha wataalamu wanaomaliza mafunzo wanakuwa na uelewa kuhusu punda na huduma zinazohitajika, akieleza kuwa awali kulikuwa na pengo katika mitaala ya mafunzo ya mifugo kuhusu mnyama huyo.

Dkt. Malinda amesema Serikali pia imeendelea kushirikiana na wadau katika kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa punda katika jamii, akieleza kuwa mnyama huyo hutumika kubeba maji, kuni na mizigo, kusaidia shughuli za kilimo na katika baadhi ya maeneo kusaidia watoto kufika shuleni, amesema pia mwitikio wa viongozi na jamii katika maadhimisho ya Siku ya Punda Duniani umeendelea kuongezeka, hatua inayosaidia kuongeza uelewa kuhusu ustawi wa mnyama huyo.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa mwongozo wa matibabu ya punda, ambao unawasaidia wataalamu kutoa huduma kwa mnyama huyo, wakiwemo wataalamu waliopata mafunzo kabla ya masuala ya punda kuingizwa katika mitaala, aidha, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti uchinjaji na biashara ya punda pamoja na mazao yake kwenda nje ya Tanzania.

Mkurugenzi wa INADES Formation Tanzania, Jacqueline Nicodemus, amesema kikao hicho kililenga kumtambua punda katika huduma za mifugo zinazotolewa nchini pamoja na kushughulikia hatua za kumtambua punda kama mnyama asiyehusika na matumizi ya chakula kupitia Gazeti la Serikali, ameeleza kuwa wamepata hakikisho kutoka Serikalini kuhusu hatua zinazoendelea za kuhakikisha wanyama kazi, akiwemo punda, wanatambuliwa katika mfumo wa huduma za afya ya mifugo, utambuzi wa mifugo na magonjwa ya mifugo.

Jacqueline amesema wamepata taarifa kuhusu mchakato wa kanuni ya uchinjaji wa kibinadamu wa wanyama, Humane Slaughter Regulation, 2024, ambao amesema umefikia hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka 2027, ameishukuru Serikali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na watendaji wa Wizara kwa ushirikiano katika kuhakikisha wanyama kazi wanatambuliwa na kupewa uzito katika mipango na bajeti zinazohusu sekta ya mifugo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la kutetea wanyama la ASPA (Arusha Society for the Protection of Animals) Livingstone Masija, amesema punda amekuwa msaidizi mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii, lakini bado anakabiliwa na changamoto ya kutopatiwa huduma za afya kama wanyama wengine, ambapo punda anahitaji matibabu, chanjo na huduma nyingine za mifugo, huku akiiomba Serikali kumtambua zaidi kama mnyama kazi na kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi na ustawi wake ili aendelee kuwa na mchango katika jamii.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...