NNa Mwandishi Wetu - Dodoma


SERIKALI imetoa maelekezo 13 kwa umma, kamati za usimamizi wa maafa, Wizara, Taasisi, Mikoa, Halmashauri na sekta mbalimbali nchini, kwa ajili ya kujiandaa na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino.

Imeelekeza maeneo yote hatarishi yatambuliwe mapema, tathmini za vihatarishi zifanyike na hatua stahiki zichukuliwe, ikiwemo kuwahamasisha wananchi kuondoka katika maeneo hatarishi na kwenda maeneo salama.

Maelekezo hayo yametolewa hii leo (02 Septemba,2026) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Nino.

Profesa Kabudi amesema Serikali imeelekeza kuhakikisha mvua hizo zinatumika kikamilifu kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi.

Aidha, amesisitiza wananchi wanapaswa kuelimishwa na kuhimizwa kuchukua hatua za kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama, kuweka akiba ya chakula, kutumia mbinu bora za kilimo na kuchagua mazao pamoja na mbegu bora kwa msimu wa Vuli.

“Kuandaa rasilimali kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa na kukabiliana na maafa yatakayotokea na kushirikisha wadau wote wa maafa, wakiwemo wananchi, taasisi na sekta binafsi katika maeneo yao,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Serikali imeagiza kuandaliwa na kutekelezwa kwa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea.”

Profesa Kabudi amesema Wizara, Taasisi, Mikoa na wadau wengine wanaohusika na miundombinu wanapaswa kufanya ukaguzi wa miundombinu muhimu na kuhakikisha inaimarishwa na kusafishwa, ikiwemo madaraja, makaravati na mitaro.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kabla, wakati na baada ya maafa kutokea, zikiwemo huduma za usafirishaji, maji na umeme.

Serikali pia imeagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa taka ngumu, usafishaji na uimarishaji wa njia za maji, kingo za mito na mabwawa.

Aidha, imeelekeza kuhakikisha vifaa vya uokoaji, huduma za dharura na mifumo ya mawasiliano vinapatikana na kuwa katika hali ya utayari wakati wote.

Katika hatua nyingine, Serikali imeagiza kubainisha na kutenga maeneo salama yatakayotumika kwa ajili ya makazi ya dharura pindi maafa yatakapotokea.

Kwa upande wa sekta ya utalii, Serikali imeagiza kufanyika kwa ukaguzi na ukarabati wa miundombinu iliyopo katika maeneo ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi za Jamii ili kuhakikisha shughuli za utalii zinaendelea wakati wote.

“Wizara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote zimeagizwa kufuatilia na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu pamoja na taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ili hatua stahiki za kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El-Nino zichukuliwe kwa wakati.”


KUHUSU BILIONI 730


Akizungumzia taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu makadirio ya matumizi ya Sh. bilioni 730 katika kujiandaa na kukabiliana na El-Niño, Profesa Kabudi amesema taarifa hiyo haikutoa ufafanuzi wa kina kuhusu shughuli zilizoainishwa katika mpango huo.

Amesema Sh. bilioni 730 ni makadirio ya fedha zinazohitajika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Niño kabla, wakati na baada ya El-Nino kutokea.

“Kwa mujibu wa Mpango, makadirio ya fedha zinazohitajika kutumika katika kutekeleza Mpango huo ni Sh. bilioni 730,” amesema.

Hata hivyo, amesema fedha zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo katika sekta zote ni Sh. bilioni 10.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...