Na Janeth Raphael -MichuziTv -Bungeni Dodoma
SERIKALI imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha taaluma na kazi ya udereva nchini zinapata staha, hadhi na heshima inayolingana na kada nyingine katika utumishi wa umma.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, wakati akijibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi (Mlalo) lililouliza kuhusu mkakati wa Serikali wa kuinua hadhi ya taaluma ya udereva.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Qwaray amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa zikiwemo kuboresha Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada ya Udereva, ili kuwawezesha watumishi wa kada hiyo kupata fursa za maendeleo ya kiutumishi.
Amesema Serikali pia inaendelea kuboresha mafunzo ya kitaaluma pamoja na viwango vya elimu kwa madereva, hatua inayolenga kuongeza weledi, ufanisi na uwezo wa watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Serikali pia imeendelea kuimarisha motisha na maslahi ya kada ya udereva, kwa kuzingatia mazingira ya kazi na mahitaji ya utendaji, ili kuhakikisha madereva wanatekeleza majukumu yao katika mazingira yanayostahili.
Hatua hizo, amesema, ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha kada ya udereva inatambuliwa na kuthaminiwa kama taaluma yenye mchango muhimu katika utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...