Taasisi za LALJI FOUNDATION na BARAKA  FOUNDATION  kwa kushirikiana na  VISION 4 ALL EYE CENTER  imeendesha Kambi ya Matibabu ya Macho Bure katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Mkoa wa Tanga, kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata huduma za uchunguzi, matibabu na upasuaji wa macho bila gharama.

Kambi hiyo iliyofanyika kwa muda wa siku tatu imewafikia jumla ya wananchi 3,259, ambao walihudhuria na kupata huduma mbalimbali za afya ya macho.

Akizungumza baada ya kutamatika kwa kambi hiyo mwenyekiti wa LALJI FOUNDATION Imtiaz Lalji amesema kwa siku zote tatu, jumla ya wagonjwa 333 walifanyiwa  upasuaji wa macho, Kati yao, 291 walibainika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho (cataract), huku 39 wakiwa na matatizo madogo ya macho yaliyohitaji huduma za upasuaji.

Aidha, jumla ya wananchi 1,723 walipewa dawa kulingana na mahitaji yao ya kiafya, huku wananchi 1,706  wakipatiwa miwani ya kusomea (reading glasses).

Imtiaz Lalji, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kuwasaidia Watanzania kupata matibabu ya macho bila malipo, kutokana na changamoto ya magonjwa ya macho ambayo imeendelea kuwaathiri wananchi wengi.

“Takwimu zilizopatikana katika kambi hiyo zinaonesha ukubwa wa changamoto ya magonjwa ya macho katika jamii, akibainisha kuwa wananchi wa maeneo ya vijijini ni miongoni mwa wanaokumbwa zaidi na changamoto ya upatikanaji wa huduma za macho kwa wakati" ameongeza

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Bi. Zahara Msangi, ameishukuru LALJI FOUNDATION na Baraka FOUNDATION  kwa kuguswa na changamoto zinazowakabili wananchi na kuamua kufikisha huduma za matibabu ya macho katika Halmashauri hiyo.

Amesema huduma hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi, hususan wale ambao wamepata fursa ya kufanyiwa uchunguzi, kupata dawa, miwani pamoja na upasuaji bila kulipia gharama.

Naye Mratibu wa Huduma za Macho Mkoa wa Tanga, Dkt. Husein Abassy, amesema kuletwa kwa huduma hiyo mkoani Tanga ni hatua muhimu inayolenga kuwafikia wananchi wenye uhitaji, hususan wale ambao wanakabiliwa na changamoto ya kupata huduma za macho kwa wakati.

Nao baadhi ya wananchi walionufaika na kambi hiyo wameeleza namna huduma hizo zilivyowasaidia kupata matibabu ambayo huenda wasingeweza kuyapata kwa urahisi kutokana na gharama.

Wameishukuru LALJI FOUNDATION kwa huduma hiyo na kutoa wito kwa taasisi nyingine, mashirika na wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika kuboresha afya na ustawi wa wananchi.

Huduma hiyo ya matibabu ya macho bila malipo ni sehemu ya juhudi za LALJI FOUNDATION  katika kusaidia jamii na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

 Taasisi hiyo imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuwafikia wananchi wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali nchini.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...