Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv 

ZAIDI ya watoto 4,200 kati ya 25,617 waliofanyiwa tathmini katika Halmashauri ya Jiji la Tanga wamebainika kuwa na changamoto katika stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), hali iliyosababisha kuanza kutumika kwa mbinu ya Teaching at the Right Level (TaRL) ili kuwasaidia kumudu stadi hizo.

Mratibu wa Mradi wa TaRL, Alex Sigalla, amesema baada ya watoto hao kufundishwa kwa kutumia mbinu hiyo, kati ya asilimia 80 na 85 waliweza kumudu stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

Sigala amesema hayo wakati kando ya  Mkutano wa Sita wa African Curriculum Association (ACA), uliofanyika Dar es Salaam, akieleza kuwa mradi huo unaotekelezwa katika shule zote 87 za Halmashauri ya Jiji la Tanga unalenga kuhakikisha hakuna mtoto anayevuka kwenda darasa la tatu bila kumudu stadi hizo.

Amesema TaRL haimwangalii mtoto kwa kuzingatia umri au darasa analosoma, bali kiwango chake cha uelewa. Hivyo, mtoto mwenye changamoto huwekwa katika kundi linalolingana na uwezo wake na kufundishwa kwa kutumia mbinu shirikishi.

“Unaweza ukaona mtoto yuko darasa la sita lakini ana changamoto za mwambatano. Huyu katika ngazi ya uelewa ana changamoto ya silabi sawasawa na yule mtoto aliyeko darasa la awali, la kwanza au la pili,” amesema.

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo, walimu 176 tayari wamejengewa uwezo wa kutumia mbinu ya TaRL, huku lengo likiwa kuwafikia walimu 261 katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Kwa mujibu wa Sigala, mafanikio yaliyopatikana Tanga yamewafanya kuendelea kuhimiza matumizi ya TaRL katika shule zote nchini, akisema mbinu hiyo inaweza kusaidia kukabiliana na changamoto ya watoto kushindwa kumudu stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

Amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kushirikiana katika hatua za kuangalia namna mbinu hiyo inaweza kusambazwa zaidi nchini.

“Kwa maana hii, tayari Wizara ya Elimu imeshakuwa tayari ni mdau mkubwa ambaye tayari anataka kuona watoto kufikia darasa la pili kwenda la tatu, hakuna mtoto atavuka kama atakuwa na changamoto za KKK,” amesema.

Kwa upande wake, Mwalimu Baturi Msuya wa Shule ya Msingi Tanga amesema TaRL imekuwa rahisi kutumia kwa kuwa inamshirikisha mtoto kupitia michezo, nyimbo na ubunifu mbalimbali.

Amesema shule zote 87 za Halmashauri ya Jiji la Tanga zimepata mafunzo hayo, huku kila shule ikiwa na walimu wawili wanaotumia mbinu hiyo kuwasaidia watoto wenye changamoto za KKK.

Msuya amesema vifaa vinavyotumika katika utekelezaji wa mbinu hiyo ni rahisi kupatikana, kwa kuwa baadhi yake hutengenezwa kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira ya kawaida, ikiwamo maboksi, makuti, vifuu vya nazi na karatasi.

Amesema matumizi ya TaRL yameongeza uwezo wa watoto katika KKK, akieleza kuwa kwa sasa zaidi ya asilimia 96 ya watoto wa darasa la pili wanaweza kusoma, kuandika na kuhesabu.

“Mbinu ambayo mtoto ndiye kitovu cha ujifunzaji. Maana yake hata ukiwa haupo, ukiacha darasa liko hivi, wanacheza wenyewe na wanajifunza wenyewe kwa wenyewe,” amesema.

Msuya  amewataka walimu wa mikoa mingine kuipokea mbinu hiyo, akisema inamwezesha mtoto kujifunza kwa kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa ujifunzaji.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...