KASI ya ukuaji wa Teknolojia ya Akili Unde (AI) imeibua mjadala kuhusu uwezo wa sera, taasisi na mifumo ya uongozi nchini kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia hiyo.
Hoja hiyo imeibuliwa katika Mkutano wa Tatu wa Vyuo Vikuu Vitano (5UCC) unaofanyika katika Taasisi ya Nelson Mandela African Institution of Science and Technology (NM-AIST), Arusha, kuanzia Septemba 23 hadi 25, 2026.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema mjadala kuhusu AI haupaswi kuangalia uwezo wa teknolojia hiyo pekee, bali pia namna taasisi, sera na mifumo ya uongozi inavyopaswa kuitikia fursa na changamoto zake.
“Huu ndio hasa aina ya mjadala tunaouhitaji, si kuhusu tu kile ambacho teknolojia inaweza kufanya, bali pia namna taasisi zetu, sera zetu na mifumo yetu ya uongozi inavyopaswa kuitikia fursa na changamoto zinazoletwa na teknolojia hiyo,” amesema.
Katika mkutano huo, Dkt. Philbert Nyinondi, mhadhiri na mtafiti wa mawasiliano ya sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amewasilisha utafiti unaochunguza uwezo wa miongozo ya AI kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia hiyo katika elimu ya juu.
Utafiti huo umechambua National Guidelines for AI in Education (NGAIE) na National Digital Education Guidelines for Universities (NDEGU), zote za mwaka 2025, na kubaini kuwa Tanzania tayari ina msingi wa kisera unaotambua ufuatiliaji, mrejesho na maboresho ya sera.
Hata hivyo, Dkt. Nyinondi amesema bado kuna mapungufu, ikiwamo kutokuwepo kwa vichocheo vilivyoainishwa wazi vya kufanya mapitio ya haraka ya sera, muda wa kushughulikia changamoto za dharura, mfumo wa tahadhari za awali kuhusu teknolojia zinazoibuka na utaratibu wa wazi wa kuunganisha taarifa za ufuatiliaji na maamuzi ya kisera.
Amesema kadiri AI inavyoendelea kubadilika, matumizi yake katika elimu ya juu yanaweza kuleta changamoto ambazo hazikutarajiwa wakati miongozo hiyo ilipoandaliwa, hivyo mifumo ya kisera inahitaji kuwa na uwezo wa kutambua mabadiliko hayo na kuchukua hatua kwa wakati.
Dkt. Nyinondi amesema hoja si kwamba Tanzania haiwezi kubadilisha sera, bali ni kama mifumo iliyopo inaweza kufanya mabadiliko hayo kwa kasi inayolingana na maendeleo ya AI.
Kwa upande wake, Profesa Raffaella Cagliano wa Politecnico di Milano, Italia, amesema maendeleo ya teknolojia yanapaswa kuendana na mahitaji na mazingira ya kijamii na kiuchumi ya watu.
“Hatuwezi kutenganisha uendelezaji wa teknolojia na uhalisia wa mazingira na mifumo ya kijamii,” amesema.
Naye Profesa Tushar Shinde wa IIT Madras Zanzibar amesema AI haipaswi kupimwa kwa ukubwa wa mifumo pekee, bali pia kwa ufanisi, upatikanaji na gharama yake.
“Lengo si kujenga mfumo mkubwa zaidi. Lengo ni kuufanya mfumo uwe mdogo, wa haraka na wa gharama nafuu,” amesema.
Amesema mustakabali wa AI unapaswa kupimwa kwa kiwango cha athari inayozalisha, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga teknolojia inayoweza kuwafikia watu wengi zaidi.
Mijadala hiyo imeonesha umuhimu wa kujiandaa kwa matumizi ya AI katika ufundishaji, ujifunzaji, tathmini, utafiti na huduma za kitaaluma, sambamba na kuimarisha uwezo wa mifumo ya kitaifa kukusanya ushahidi, kufanya maamuzi na kurekebisha sera kwa wakati.




.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...