Wakulima katika Wilaya za Kondoa, Chemba na Bahi mkoani Dodoma wanatarajiwa kunufaika na taarifa sahihi za kiwango cha mvua zitakazonyesha kuanzia msimu ujao, kupitia vifaa vya kisayansi vilivyowekwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la  INADES-Formation Tanzania, hatua inayolenga kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kilimo, kuongeza uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa INADES-Formation Tanzania, Bi. Jacqueline Nicodemus, amesema  changamoto kubwa iliyobainika katika utekelezaji wa mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi katika sehemu kame unaotekelezwa na shirika hilo katika Wilaya za Bahi, Chemba na Kondoa, ni taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutowafikia wakulima kwa namna inayowawezesha kuzitumia moja kwa moja katika mashamba yao.

Ameeleza kuwa taarifa nyingi huishia katika ngazi za wilaya na maeneo makubwa, wakati wakulima wanahitaji taarifa zinazohusiana na maeneo yao mahsusi, na kupitia ushirikiano na TMA, vifaa vya kisayansi vya kupima mvua vimewekwa katika vijiji mbalimbali, ikiwemo Kisima cha Ndege, Gwandi na Potea, ili kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za kiwango cha mvua na kuunganisha taarifa hizo na maarifa ya asili waliyonayo, ili kuwawezesha kufanya maamzi sahihi kwenye kilimo.

Kwa upande wake, Meneja wa TMA Kanda ya Kati Mussa Kidato,  amesema vifaa vya kupima mvua vilivyowekwa, vitawawezesha wakulima kupima kwa usahihi kiasi cha mvua inayonyesha badala ya kutegemea vipimo vya asili ambavyo havina uhakika wa kutoa takwimu sahihi, amesema taarifa hizo zitawasaidia wakulima kufanya maamuzi ya mazao gani walime, huku TMA ikiendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo.

Akizungumzia manufaa ya hatua hiyo, Elizabeth Shoo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kondoa na Afisa Kiungo wa Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotekelezwa na INADES-Formation Tanzania, amesema kipima mvua kitasaidia kufuatilia kiwango cha mvua kwa kupima na kurekodi taarifa kila siku, wiki na mwezi, ambapo taarifa hizo zitawawezesha wananchi kupanga shughuli za kilimo kwa uhakika zaidi, kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mvua kubwa na kuongeza tija katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Afisa Mradi kutoka INADES-Formation Tanzania, Paul Chugu, amewataka wananchi kutunza vifaa hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa usahihi ili viweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa, aidha amewataka wananchi waliopewa mafunzo ya kupima na kurekodi taarifa za mvua kuwa makini katika kutekeleza jukumu hilo, ili kuhakikisha takwimu zinazokusanywa ni sahihi na zinatumika ipasavyo katika kupanga shughuli za kilimo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Potea Amina Juma Lungi, amesema kifaa hicho kitawasaidia wakulima kuachana na utegemezi wa vipimo vya asili na kupata taarifa sahihi za kiwango cha mvua, zitakazowawezesha kupanga shughuli zao za kilimo kwa ufanisi na kuongeza mavuno, ameahidi kuwa wananchi wa kijiji hicho watakitunza na kukitumia ipasavyo ili kiwe na manufaa kwa jamii.

Kwa ujumla, ushirikiano kati ya INADES-Formation Tanzania na TMA unalenga kuziba pengo la upatikanaji wa taarifa sahihi za mvua katika ngazi ya mkulima, kwa kuhakikisha takwimu zinazopatikana kupitia vipimo vya kisayansi zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa namna inayoeleweka, Hatua hiyo inatarajiwa kuwawezesha wakulima kufanya maamuzi bora ya kilimo, kuongeza uzalishaji na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...