Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepiga marufuku matangazo ya dawa zinazotumika kupunguza au kusaidia kuacha unywaji wa pombe, ikiwemo Naltrexone, Acamprosate na Disulfiram.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Septemba 27, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, mamlaka hiyo imebaini kuwa baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vimekuwa vikirusha na kuchapisha matangazo ya dawa hizo, ambazo kisheria ni dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari pekee (Prescription-Only Medicines – POM).

TMDA imesema hali hiyo ni kinyume cha Kanuni ya Makundi ya Dawa ya Mwaka 2026 (Tangazo la Serikali Na. 150).

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, matumizi ya dawa hizo bila ushauri na uangalizi wa mtaalamu wa afya yanaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo kifo, hasa zinapotumiwa pamoja na pombe au dawa nyingine.

“Kifungu cha 52 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, kinakataza kutangaza kwa umma dawa yoyote inayotolewa kwa cheti cha daktari. Dawa hizo zinaruhusiwa kutangazwa kwa wataalamu wa afya pekee kupitia majarida ya kitaalamu,” imeeleza taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, TMDA imewaelekeza wafanyabiashara, watoa huduma za afya, wamiliki wa vyombo vya habari na waendeshaji wa mitandao ya kijamii kuacha mara moja kuandaa, kurusha au kuchapisha matangazo ya dawa hizo.

Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa TMDA wanapobaini watu, vituo au vyombo vinavyohusika na matangazo ya dawa hizo, kupitia ofisi za mamlaka hiyo zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...