Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Stadi (VETA) imeeleza kuwa inaweka mkazo katika kuandaa vijana wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya madini, ikiwemo uendeshaji wa mitambo na shughuli nyingine za kitaalamu katika uchimbaji.

Akizungumza  Septemba 29, 2026, katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Afisa Mkuza Mitaala VETA Makao Makuu, Mhandisi Audiface Tarimo, amesema ushirikiano huo umewezesha VETA kutambua ujuzi unaohitajika katika sekta ya madini na kuandaa programu za mafunzo zinazowawezesha vijana kushiriki katika shughuli mbalimbali za uchimbaji na uzalishaji.

Amesema VETA pia imekuwa ikiimarisha uwezo wa wakufunzi kwa kushirikiana na wadau, ambapo baadhi ya walimu wamepelekwa nchini Finland kwa ajili ya kupata mafunzo, huku wakirejea na kuwajengea uwezo walimu wengine nchini.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya wakufunzi wenye uwezo wa kutoa mafunzo kwa vijana wengi zaidi wanaohitaji ujuzi unaohusiana na sekta ya madini.

Kwa upande wa vijana, Tarimo amesema VETA inawapa fursa ya kusoma kozi zinazohusiana na sekta ya madini, ikiwemo kozi za kutengeneza na kuendesha mitambo, kutokana na fursa zilizopo katika sekta hiyo na mchango wake katika uchumi wa nchi.

Aidha, amesema VETA kwa kushirikiana na Chama cha Watoa Huduma katika Sekta ya Madini Tanzania, imeandaa mitaala sita mipya inayolenga kutoa ujuzi unaohitajika katika shughuli za madini.

Mitaala hiyo ni Bogie Operation, Jumbo Operation, Solo Operation, Cubex Operation, Charge Up Operation pamoja na Lifting and Rigging.

Amesema VETA inatarajia kuanza kutoa mafunzo ya mitaala hiyo katika Chuo cha VETA Moshi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwaandaa vijana kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta ya madini.

Kwa Ujumla, VETA inalenga kuendelea kuoanisha mafunzo ya ufundi na mahitaji halisi ya sekta ya madini, ili kuongeza upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika na kuwawezesha vijana kunufaika na fursa zinazotokana na shughuli za madini nchini.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...