Na Janeth Raphael - MichuziTv
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kuimarisha mafunzo yanayolenga kuwaandaa Watanzania wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta ya madini, ikiwemo teknolojia za kisasa zinazotumika katika uchimbaji na uchakataji wa madini.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema sekta ya madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake katika pato la Taifa, uwekezaji, ajira pamoja na maendeleo ya viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali za nchi.
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma Septemba 4, 2026, Kasore amesema maendeleo ya sekta ya madini hayawezi kutegemea uwepo wa rasilimali pekee, bali yanahitaji pia wataalamu wenye uwezo wa kutumia, kutengeneza na kusimamia teknolojia na mitambo inayotumika katika migodi ya kisasa.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi katika sekta hiyo, mwaka 2008 VETA kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) ilianzisha Programu ya Mafunzo ya Ufundi kwa Shughuli za Uchimbaji Madini (Integrated Mining Technical Training - IMTT) katika Chuo cha VETA Moshi.
Kupitia programu hiyo, VETA imekuwa ikitoa mafunzo katika fani mbalimbali zinazohitajika kwenye sekta ya madini, zikiwemo Heavy Moving Equipment Mechanics, Fitting and Machining, Plater Welding, Auto Electrical na Industrial Electrical Installation.
Kasore,amesema tangu kuanzishwa kwa programu hiyo, zaidi ya vijana 1,688 wamepata mafunzo huku jumla ya kampuni 17 zikishiriki katika utekelezaji wa programu hiyo.
Hata hivyo, amesema mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya madini yamelazimu VETA kuendelea kuboresha mafunzo yake ili kuhakikisha ujuzi unaotolewa unaendana na mahitaji halisi ya migodi ya kisasa, hususan matumizi ya mitambo ya uchimbaji chini ya ardhi.
Katika hatua hiyo, VETA kwa kushirikiana na TCM imeandaa mitaala sita mipya ya mafunzo ya uchimbaji madini chini ya ardhi, ambayo inalenga kuwaandaa vijana katika matumizi na uendeshaji wa vifaa na mitambo ya kisasa.
Mitaala hiyo inahusisha Bogger Equipment Operation, Jumbo Equipment Operation, Long Hole Drill Rig, Cubex (ITH) Equipment Operation, Underground Charge-Up Operation pamoja na Lifting and Rigging Operations.
Kasore amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa ukuaji wa sekta ya madini unatoa nafasi kubwa zaidi kwa Watanzania wenye ujuzi kushiriki katika shughuli mbalimbali za uchimbaji, huku wakinufaika na fursa za ajira zinazotokana na maendeleo ya sekta hiyo.
Aidha, VETA inaendelea kutekeleza Mradi wa Madini Muhimu (Critical Minerals Project) kwa kushirikiana na taasisi za GTK na REDU Edu kutoka Finland, pamoja na ASNL ya Tanzania inayowakilisha sekta binafsi.
Mradi huo unatarajiwa kuwafikia vijana wapatao 400 kupitia mafunzo yanayohusu uchimbaji, uchakataji pamoja na ukuzaji wa mnyororo wa thamani katika sekta ya madini muhimu.
Kasore amesema hatua za awali za mradi huo tayari zimeanza, ambapo wakufunzi 25 wa VETA wamepatiwa mafunzo ya wiki sita nchini Finland na kwa sasa wanaendelea kupata mafunzo katika migodi mbalimbali nchini Tanzania kwa lengo la kuongeza uelewa wa mazingira na mahitaji ya sekta hiyo nchini.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga uwezo wa VETA kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji mahsusi ya uchimbaji na uchakataji wa madini muhimu, sambamba na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Mkurugenzi huyo amewataka wadau wa sekta ya madini, hususan kampuni za uchimbaji, watengenezaji na wasambazaji wa mitambo na vifaa vya migodini pamoja na taasisi nyingine zinazohusika katika mnyororo wa thamani, kuendelea kushirikiana na VETA katika kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika.
Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini, kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa na kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo unaendelea kuchangia katika ajira, uzalishaji na maendeleo ya Taifa.


.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...