Na Janeth Raphael – MichuziTv, Bungeni Dodoma


WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto zinazokwamisha ufanisi wa sekta ya madini, ikiwemo tozo zinazotozwa zaidi ya viwango vilivyoainishwa kisheria.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Septemba 4, 2026, wakati akilihutubia Bunge kabla ya kuahirishwa kwa shughuli zake hadi Oktoba 27, 2026, akisisitiza kuwa sekta ya madini imeendelea kuwa miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi na mapato ya Taifa.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mageuzi yanayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na ushiriki wa wadau mbalimbali wa sekta ya madini.

“Sekta ya madini imekuwa moja ya sekta kinara inayochangia katika mapato ya Taifa,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema pamoja na mchango wa wachimbaji wakubwa, wachimbaji wadogo wameendelea kuongeza uzalishaji wa madini siku hadi siku, hali ambayo imechangiwa na juhudi za Serikali katika kuweka mazingira wezeshi kwa Watanzania kushiriki na kunufaika na rasilimali hizo.

Hata hivyo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inatambua kuwa bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo, akitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni baadhi ya tozo zinazowatozwa wachimbaji wa madini katika maeneo mbalimbali.

Amesema baadhi ya tozo hizo zinahusisha malipo ya huduma yanayozidi kiwango kilichoainishwa katika Sheria ya Madini, hali ambayo imekuwa ikileta malalamiko miongoni mwa wachimbaji.

“Kwa mujibu wa sheria, kuna viwango vilivyowekwa. Hivyo, niwaelekeze Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI wakae kwa haraka kuziangalia changamoto hizo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Madini kuchukua hatua kali kwa watu wanaoshikilia leseni za uchimbaji kwa muda mrefu bila kuendeleza maeneo waliyopewa, akisema hali hiyo inawanyima Watanzania wengine, hususan vijana na wachimbaji wadogo, fursa ya kushiriki katika shughuli za uchimbaji.

Amesema kushikilia leseni bila kuendeleza maeneo husika ni kinyume na matakwa ya sheria na kwamba Serikali haiwezi kuruhusu maeneo yenye rasilimali kubaki bila kuzalisha huku wananchi wengine wakikosa fursa za kuyatumia.

“Yeyote anayetaka leseni yake isifutwe, atimize masharti yaliyowekwa kwenye leseni, aiendeleze na awape nafasi vijana wengine wa Kitanzania kufanya shughuli za uchimbaji,” amesisitiza.

Dkt. Mwigulu amemwelekeza Waziri wa Madini kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kufuta vibali na leseni za wale watakaokiuka masharti na kugawa upya maeneo hayo kwa Watanzania wenye uwezo na nia ya kuyaendeleza.

Amesema hatua kama hizo tayari zimewahi kuchukuliwa na Rais Samia katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo leseni zilizoshikiliwa bila kuendelezwa zilifutwa na maeneo hayo kupewa waombaji wengine.

Waziri Mkuu, amesema hatua hizo zimekuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kuongezeka kwa uzalishaji, mapato na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia sekta hiyo kwa kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika ipasavyo na kutoa manufaa kwa Taifa pamoja na kutoa fursa kwa Watanzania, hususan vijana na wachimbaji wadogo, kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...