Na Vero Ignatus – Michuzi TV, Arusha
WAKAGUZI wa ndani wanapaswa kuwa wataalamu wanaosaidia taasisi kuelewa vihatarishi, kutambua fursa za maboresho, kuimarisha udhibiti wa utendaji na kuongeza thamani, huku uaminifu, ukweli, ubora, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali vikiwa rasilimali muhimu katika taasisi za umma na binafsi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Ikulu) Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 19 wa Mwaka wa Ukaguzi wa Ndani pamoja na Jukwaa la 13 la Utawala Bora jijini Arusha.
Akimwakilisha Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alisema ukaguzi wa ndani unapaswa kuwa sehemu muhimu ya kufanya maamuzi na kuboresha utendaji badala ya taarifa zake kusomwa wakati wa vikao pekee.
Dkt. Mkuya alisema ni vyema kutambua kwamba rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi, tija na kuzingatia thamani ya fedha. Aliongeza kuwa jukumu la wakaguzi halipaswi kuishia katika kuthibitisha taratibu, kanuni na mifumo iliyowekwa tu, bali wanapaswa kujiuliza kama ukaguzi na mifumo hiyo ya utawala inazalisha thamani inayokusudiwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mkuya, kaulimbiu ya mkutano huo inayosisitiza kwenda “Beyond Assurance” inalenga kuwakumbusha wakaguzi wa ndani kwamba wajibu wao hauishii katika kutoa uhakikisho pekee, bali wanapaswa pia kutoa maarifa, ushauri na mtazamo wa kitaalamu unaosaidia taasisi kuboresha utendaji na kufikia malengo yake.
We wewe ndiye mwenye dhamana ya UKAGUZI wa ndani na kuangalia namna ambayo matumizi ya fedha na uratibu bora,kushauri namna gani kuwe na matumizi bora ili taasisi iende mbele. Alisema Dkt. Mkuya
Dkt. Mkuya aliongeza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha kada ya ukaguzi wa ndani, ikiwemo kuandaa sheria mahususi ya ukaguzi wa ndani itakayoweka msingi wa kisheria na kitaasisi wa kulinda uhuru, mamlaka na uwajibikaji wa wakaguzi wa ndani pamoja na kamati za ukaguzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mkutano huo, Benedicto Baragomwa, alisema mkutano huo unawakutanisha wakaguzi wa ndani, viongozi wa bodi, watendaji wa taasisi, wataalamu wa vihatarishi, sekta binafsi na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Baragomwa alisema mazingira ya utendaji yameendelea kubadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia, ongezeko la vihatarishi vya usalama wa mtandao, mabadiliko ya sheria na mahitaji ya wananchi; hivyo wakaguzi wa ndani wanapaswa kuwa na uwezo wa kutazama mbele na kutoa ushauri unaoendana na mabadiliko hayo.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA Tanzania), Jonathan Ngoma, amezishukuru Wizara ya Fedha ya Muungano, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, taasisi za serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wadhamini kwa kushiriki katika maandalizi ya mkutano huo.
Ngoma alisema mkutano huo unatoa fursa kwa wataalamu kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya na kujadili namna ya kuimarisha utawala bora, usimamizi wa vihatarishi na uwajibikaji katika taasisi, pamoja na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya taifa.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...