
Na Oscar Assenga, TANGA
KAIMU Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Emidius Kasunzu, amesema maendeleo ya sekta ya Usafiri majini yanahitaji kuwa na wataalamu, wabunifu, wajasiriamali na watafiti wenye uwezo wa kutambua changamoto na kuzigeuza kuwa fursa za maendeleo.
Amesema Tanzania inapaswa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko makubwa yanayoendelea katika sekta ya usafiri wa majini, ikiwemo matumizi ya nishati safi, teknolojia za kidijitali na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa bandari.
Alitoa kauli hiyo jijini Tanga wakati akifungua warsha ya Siku ya Bahari Duniani 2026, iliyolenga kujadili namna ya kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kimataifa na kitaifa vinavyosimamia sekta ya usafiri wa majini.
Amesema miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika warsha hiyo ni kuimarisha usalama na ufanisi wa shughuli za usafiri wa majini, matumizi ya nishati safi na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa katika meli na bandari.
Pia amesema warsha hiyo inalenga kujadili namna ya kuimarisha ustawi, usalama na hifadhi ya kijamii kwa mabaharia, kuwaandaa wataalamu kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia yanayokua kwa kasi pamoja na kuboresha mafunzo na maendeleo ya rasilimali watu.
Kwa mujibu wa Kasunzu, lengo ni kujenga sekta ya usafiri wa majini yenye ufanisi, usalama na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesisitiza kuwa mijadala inayofanyika katika warsha hiyo haipaswi kuishia katika kubainisha changamoto pekee, bali inapaswa kuzaa hatua mahususi zitakazowezesha utekelezaji wa suluhisho.
“Warsha hii inapaswa kuwa na matokeo ya vitendo,” amesema.
Kasunzu amesema sekta ya usafiri wa majini kwa sasa inapitia mabadiliko makubwa yanayochangiwa na matumizi ya nishati safi, maendeleo ya teknolojia za kidijitali, mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa bandari pamoja na mahitaji mapya ya ujuzi kwa mabaharia.
Amesema mabadiliko hayo, pamoja na kuleta changamoto, yanatoa fursa kubwa kwa Tanzania, hivyo nchi haiwezi kubaki mtazamaji wakati dunia ikiendelea kubadilika.
“Tanzania haiwezi kubaki kuwa mtazamaji wa mabadiliko haya. Tunapaswa kujiandaa kuyatumia kwa manufaa ya Taifa letu na kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.
Amesema maandalizi hayo yanapaswa kuzingatia mazingira ya Tanzania, uzoefu uliopo pamoja na mahitaji ya wananchi, huku rasilimali watu ikiwa msingi muhimu wa kufanikisha mabadiliko hayo.

Kasunzu amesema teknolojia mpya zinahitaji wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya sekta, akieleza kuwa meli za kisasa zinahitaji mabaharia walioandaliwa kwa viwango vya kisasa.
Ameongeza kuwa bandari za kisasa nazo zinahitaji wataalamu wenye uwezo wa kusimamia, kuendesha na kuboresha mifumo ya kiteknolojia ili kuongeza ufanisi wa shughuli za usafiri na biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi Zanzibar, Stella Katondo, amesema maadhimisho hayo pamoja na warsha yameandaliwa kwa lengo la kuhakikisha masuala ya ulinzi, usalama na uhifadhi wa mazingira katika sekta ya usafiri wa majini yanapewa kipaumbele.

Katondo amesema ni muhimu kuhakikisha bahari, mito na vyanzo vingine vya maji vinatumika kwa namna ambayo haitawanufaisha watu wa kizazi cha sasa pekee, bali pia vinahifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Amesema Shirika la Kimataifa la Usafiri Majini (IMO) huweka miongozo mbalimbali ya usalama, ulinzi na uhifadhi wa mazingira ambayo Tanzania, kama mwanachama, inapaswa kuifuata na kuitekeleza.

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasisitiza umuhimu wa kutoka katika hatua ya kutunga sera na kuelekea katika utekelezaji wake kwa vitendo.
Kwa mujibu wa Katondo, utekelezaji huo unahitaji wataalamu wenye weledi na uwezo wa kuhakikisha masuala ya ulinzi, usalama na uhifadhi wa mazingira yanazingatiwa ipasavyo katika shughuli za usafiri wa majini.

Amesema kamati ya maandalizi imeandaa mada mbalimbali zinazolenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa ulinzi, usalama na uhifadhi wa mazingira.
Katondo amesema makundi mbalimbali yamehusishwa katika shughuli hizo, wakiwemo wanafunzi ambao amewataka kuwa mabalozi wa kuhamasisha wenzao, vijana, walimu na wazazi kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na kuzingatia usalama katika shughuli za usafiri wa majini.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (TASAC), Judith Kakongwe, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, amesema warsha hiyo pia inatoa nafasi kwa Tanzania kutafakari utekelezaji wa mikataba ya kimataifa katika maeneo ya usalama, mazingira na mabaharia.
Kakongwe amesema Tanzania imeridhia mikataba 25 kati ya mikataba 50 ya kimataifa inayosimamia sekta hiyo na kwamba inaendelea kupitia mikataba mingine ili kuhakikisha nchi haiwi nyuma katika utekelezaji wa viwango vinavyotumika kimataifa.

Amesema mikataba ambayo Tanzania imeridhia imewezesha kutengenezwa kwa sheria na kanuni mbalimbali zinazosaidia kusimamia sekta hiyo.
“Tunatoa elimu, tunatafakari na kufanya tathmini ya sheria tulizonazo, ikiwemo katika usajili wa meli, mabaharia, elimu zao na utekelezaji wa majukumu katika maeneo ya mazingira,” amesema.

Kakongwe amesema TASAC ina sheria 64 zinazotekeleza mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, hivyo tathmini inayofanyika inalenga kuhakikisha sheria hizo zinatekelezwa kwa ufanisi na matokeo yake yanaonekana kwa wananchi.
Amesema moja ya hatua zinazochukuliwa ni kuhakikisha huduma za usafiri wa majini zinakuwa na uwezo wa kutoa msaada wa haraka pale ajali zinapotokea.

Ametoa mfano wa hatua za kupeleka boti katika maeneo mbalimbali ya Maziwa Makuu kwa ajili ya kusaidia katika matukio ya dharura, akisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata msaada kwa wakati na kupunguza madhara kwa maisha na mali.
Kwa ujumla, warsha hiyo inalenga kujenga uelewa, kuibua suluhisho na kuweka mikakati ya kuhakikisha sekta ya usafiri wa majini nchini inaendana na mabadiliko ya teknolojia, viwango vya kimataifa pamoja na wajibu wa kulinda mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...