Wanariadha wa Kenya wametawala mbio za kilomita 21 za Yas Zanzibar International Marathon 2026, huku Watanzania waking’ara katika kilomita 10 kwenye msimu wa sita wa mashindano hayo yaliyofanyika Viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Katika kilomita 21 kwa upande wa wanaume, Wakenya Justus Nyesya, Ransisi Kamito na Simon Kelenzyo walishinda nafasi zote tatu za juu na kwa upande wa wanawake, Valentine Chep na Rael Mitieka wa Kenya wakimaliza nafasi ya kwanza na ya pili, huku Mtanzania Failuna Abdi akichukua nafasi ya tatu.

Kilomita 10 kwa wanaume ilitawaliwa na Watanzania Shedrak Damas na Boay Maganga, huku Duncan Kipchumba wa Kenya akishinda nafasi ya tatu. Kwa upande wa wanawake, nafasi ya kwanza ilienda kwa Mkenya Bi. Faith Jeptum akifuatiwa na Watanzania Anna Dolomong na Dorcas Boniface.

Akifunga mashindano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma ambaye alimwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alisema kuwa mbio hizo zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza michezo na kuitangaza Zanzibar kupitia utalii.

“Mashindano haya yana mchango mkubwa katika kukuza michezo na kuitangaza Zanzibar kama moja ya maeneo muhimu ya utalii, huku yakifungua fursa katika sekta za hoteli, usafiri, biashara na huduma mbalimbali,” alisema Mhe. Juma.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura, alisema katika kipindi cha miaka sita, mbio hizo zimekua sehemu muhimu ya kuitangaza Zanzibar, kuhamasisha mtindo bora wa maisha yenye afya na kuchochea uchumi wa buluu.

Alisema Yas imeendelea kuwekeza Zanzibar, ambapo mtandao wake umeenea kwa takriban asilimia 99 Zanzibar, huku zaidi ya minara mipya 60 mipya ikikamilishwa mwaka huu kwa kushirikiana na Serikali na UCSAF. Kupitia Yas Fiber, kampuni pia imeingia makubaliano na ZICTIA kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 300 katika miundombinu ya fiber.

Rwetabura aliongeza kuwa kwa upande wa Mixx, Kampuni hiyo imeendelea kuimarisha huduma za fedha kidijitali Zanzibar, ikiwemo kurahisisha usajili na malipo ya mbio hizo kwa watanzania, kurahisisha huduma kwa wakulima kupitia kwa kushirikiana na ZSTC huku ushiriano na ZanBus, ukirahisisha malipo ya nauli kidigitali kwa wakazi wa Zanzibar. 

Alisema pia kuwa Mixx imeendelea kufanya mashirikiano mbalimbali na taasisi kiswani humo ikiwemo ushirikiano wa hivi karibuni na ZANGOF pamoja na ZMBF unaolenga kupanua huduma za kidijitali kwa makundi mbalimbali, yakiwemo ya wakulima wa mwani.

Yas pia imeendelea na programu za kijamii Zanzibar, ikiwemo kutoa intaneti bila malipo katika shule zaidi ya 50 za Serikali, kambi za huduma za macho na Kampeni ya Tumaini inayosaidia huduma za afya ya mama na mtoto.

Mashindano hayo yalihusisha mbio za kilomita 21, 10 na 5, yakileta pamoja wanariadha kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...